NA FATMA AYOUB, MCC

JESHI la Polisi kikosi cha Usalama barabarani, limemfikisha mahakamani mshitakiwa Bele Mohammed Ibrahim (30) mkaazi wa Magomeni Unguja, kwa kosa la kuendesha chombo cha moto akiwa hana bima.

Alidaiwa kutenda kosa hilo kinyme na kifungu cha 3 (1) (2) cha sura nambari 136 cha sheria za bima Zanzibar.

Alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe iliyopo Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ilidaiwa mahakanani hapo, mshitakiwa huyo alifanya kosa hilo Agosti 5 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi huko Fuoni Polisi Magharibi ‘B’ Unguja.

Siku hiyo alidaiwa kukamatwa akiwa anaendesha Honda yenye nambari za usajili Z 939 BL akitokea upamde wa Fuoni meli tano kuelekea Jumbi Sokoni, ambapo kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo akiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Suleiman Jecha Zidi, alisomewa shitaka lake lililomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Mwalim Gharib.

Baada ya kusomewa shitaka lake hilo, Bele aliiomba mahakama imsamehe kwa kudai kuwa ndilo kosa lake la kwanza kulifanya, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kubukumbu na kosa jengine kwa mshitakiwa huyo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Suleiman baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, alimtoza mshitakiwa faini ya shilingi 20,000 au kwenda kutumikia Chuo cha Mafunzo muda wa wiki moja ikiwa hakulipa, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaopuuza sheria za njia, faini ambayo aliilipa.