NA HUSNA SHEHA

KUKU jike mwenye rangi nyekundu, amemburuza mahakamani Khamis Wadi Mati (20) mkaazi wa Bumbwini Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Kuku huyo amempandisha mshitakiwa huyo katika kizimba cha mahakama ya Wilaya Mfenesini, mbele ya Hakimu Zuwena Mohammed.

Akisoma hati ya mashitaka kwa mshitakiwa huyo, Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Raghida Said.

Alidai mahakamani hapo kwamba, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 8 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi huko Bumbwini Kidanzini Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Kwa mujibu wa maelezo yaliotolewa Mahakamani hapo na wakili huyo alidai kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana akiwa ameiba kuku mmoja jike rangi nyekundu.

Wakili huyo alidai kuwa Kuku huyo alikuwa na thamani ya shilingi 10,000 kwa makisio ikiwa ni mali ya Shafiuna Saleh Korozi.

Mshitakiwa alifikishwa makamani hapo kwa kosa la wizi wa mazao, ambapo kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 251 (1) 268 (1) (2) (3) sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Hata hivyo mshitakiwa alikana kosa hilo na huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika.

Mshitakiwa huyo amepelekwa rumande hadi Agosti 24 mwaka huu kwa kusikiliza mashahidi.