NA KHAMISUU ABDALLAH
DEREVA aliyedaiwa kupakia abiria gari ikiwa na mwendo, amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.
Mshitakiwa huyo ni Seif Juma Ali (27) mkaazi wa Amani wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mohammed Ali Haji na kusomewa mashitaka yanayomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Time Said.
Alidaiwa kuwa, kosa la kwanza alilopatikana nalo ni kutotii sheria za njia, kinyume na kifungu cha 143 cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa, Julai 26 mwaka huu saa 9:30 jioni huko Amani, akiwa dereva wa gari namba Z 501 KK inayoenda njia 513 akitokea Amani kwenye mzunguko wa barabara kuelekea Welezo, alipatikana akiwa amesimamisha gari katikati barabara na kupakia abiria kitendo ambacho ni kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara.
Kosa la pili alilopatikana nalo mshitakiwa huyo ni kuchukua watu kwa njia ya hatari, kinyume na kifungu 121 (5) (6) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Mshitakiwa Seif, alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo katika maeneo hayo alipatikana akiwa amemchukua abiria huku gari ikiwa kwenye mwendo na kusababisha hatari, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Aliposomwa mashitaka hayo aliyakubali na kuiomba mahakama imsamehe kwa madai kuwa ndio makosa yake ya mwanzo.