NA KHAMISUU ABDALLAH

ABDALLA Saleh Saadat (25) mkaazi wa Amani, amefikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe akikabiliwa na mashitaka mawili tofauti ikiwemo la wizi.

Mshitakiwa huyo, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mummin Ali Juma na kusomewa mashitaka yanayomkabili na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nassra Khamis.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kwanza la kuvunja nyumba usiku na kuingia ndani kwa dhamira ya kutenda kosa, kinyume na kifungu cha 291 (a) (2) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheriza Zanzibar.

Alidaiwa kuwa Januari 20 mwaka huu saa 11:30 alfajiri huko Nyerere, alivunja nyumba usiku na kuingia ndani ya anayoishi Issa Abdalla Ali kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kosa la pili ni wizi, kinyume na kifungu 251 (1) (2) (a) na 258 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Wakili Nassra alidai kuwa, siku hiyo hiyo mshitakiwa huyo aliiba TV moja aina ya JVC ‘flat screen’ ya inchi 19, DVD aina ya Singsong, pasi moja ya umeme pamoja na flash moja, vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi 250,000 kwa makisio mali ya Issa Abdalla Ali, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa mashitaka hayo aliyakataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo halikuwa na pingamizi mahakamani hapo.

Wakili Nassra alidai kuwa, upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 100,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima cha shilingi 50,000 fedha taslimu kila mmoja, barua ya Sheha na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.