NA TATU MAKAME
TWALIB Adinani Olomi (29) mkaazi wa Mkele Wilaya ya Mjini Unguja, aliyekuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwenye namba 141 KJ aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kuuwa kwa makusudi, ameachiwa huru na mahakama ya mkoa wa Vuga.
Sababu ya kuachiwa huru mshitakiwa huyo ni kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa juu ya kosa alilodaiwa kutenda.
Mshitakiwa huyo alidaiwa kumuua Khamis Mustapha Iddi aliachiwa huru chini ya kifungu cha 95 (1) sheria namba 7 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.
Mshitakiwa huyo alidaiwa kutenda kosa hilo Aprili saba 2014 majira ya saa 10:30 usiku Kidimni Wilaya ya Kati Unguja.
Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo mshitakiwa huyo alimuua kwa kumpiga ngumi na mateke marehemu hadi kufa wakati mshitakiwa huyo akiwa amevalia sare za kijeshi, jambo ambalo ni kosa.
Jaji wa mahakama hiyo Abraham Mwampashe alimuachia huru mshitakiwa baada ya kushindwa kuthibitika kosa hilo.
Hata hivyo jumla ya mashahidi 12 walifika kutoa ushahidi lakini upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha kosa na mshitakiwa kuachiwa huru.