NA KHAMISUU ABDALLAH

BAADA ya mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa mshitakiwa Fetu Sadik (30) mkaazi wa Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, hatimae akamatwa Julai 23 na kufikishwa mahakamani kuendelea na kesi yake.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe Julai 25 mwaka huu, mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Mwendesha Mashitaka, Sajenti wa Polisi Hassan Mussa Mshamba, aliiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi akiwemo daktari.

Hakimu Nassem, alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Mshitakiwa huyo anakabiliwa na shitaka la shambulio la kuumiza mwili, kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka Sajenti wa Polisi Hassan Mussa Mshamba, mshitakiwa huyo alimshambulia Halima Nassor Msanif, kwa kumpiga kifimbo cha kusukumia chapati sehemu ya kichwani na kumtafuta kidole cha shahada mkono wa kulia, na kumsababishia maumivu makali jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Disemba 21 mwaka jana, majira ya saa 5:00 usiku huko Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.