NA ARAFA MOHAMED
MTU mmoja amefikishwa katika mahakama ya Mwanzo Mwanakwerekwe, kujibu tuhuma za kushindwa kuvaa beji ya utingo.
Mshitakiwa huyo ni Machano Issa Khamis (25) mkaazi wa Donde Unguja, amefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nassim Fakih Mfaume na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Salum Ali.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo akiwa utingo wa gari yenye namba za usajili Z 381 CR,inayokwenda njia namba 121,ukitokea upande wa Mtoni kuelekea Muembemakumbi, alipatikana akiwa hakuvaa beji ya utingo, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Tukio hilo alidaiwa kulitenda Julai 25 mwaka huu, majira ya saa 3:28 asubuhi, huko Maruhubi Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Kosa la kutokuvaa beji ya utingo ilidaiwa kuwa ni kinyume na kifungu cha 99(6) (14) sheria ndogo za magari ya biashara, chini ya kifungu cha 80 cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Aliposomewa shitaka lake hilo mshitakiwa huyo, alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe, ombi ambalo halikukubaliwa mahakamani hapo.
Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 20,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine watakao dharau sheria za usalama barabarani.
Mshitakiwa Machano alifanikiwa kulipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo kama alivyoamriwa na Hakimu Nassim.