LONDON, England

PIERRE-Emerick Aubameyang ameibuka na kusema kwamba bado hajapewa ofa yoyote ya mkataba mpya na klabu yake ya Arsenal.

Takribani wiki sasa imekuwa ikielezwa kwamba mshambuliaji  huyo yupo kwenye mazungumzo na klabu yake, ambayo imemuandalia mkataba mpya wa miaka mitatu, kuendelea kusalia ndani ya viunga vya Arsenal ambapo kwa wiki atakuwa akilipwa pauni 250,000.

Aubameyang amebakiwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake ndani ya Arsenal na kumekuwa na maneno mengi kwamba amekubali kuongeza mkataba mpya, huku taarifa nyingine zikisema anataka kuondoka.

Hivi karibuni, Aubameyang alikuwa akizungumza na mashabiki wake ‘live’ kupitia akaunti yake ya Instagram, akiwa sambamba na kaka yake, Willy, ambapo mshambuliaji huyo alisema: “Kila mmoja anaonesha peni na karatasi, lakini binafsi sina karatasi.”

Maelezo yake hayo yanamaanisha kwamba bado hajasaini na wala hajapewa ofa mpya na Arsenal.