NA MADINA ISSA

MKUU wa moa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka waumini wa dini ya kiislamu kusherehe mwaka mpya wa kiislamu wa 1442 kwa kujifunza mambo mema ikiwemo historia ya dini yao na historia za viongozi wa dini hiyo.

Akizungumza na walimu, wanafunzi na waumini wa dini hiyo katika kituo cha maendeleo cha Almadarasatul Twariqatul Irshaad, Tunguu mkoani humo katika sherehe za kusheherekea mwaka mpya wa kiislamu, alisema kufanya hivyo kutaongeza na kuimarisha Imani zao.

Alisema endapo waumini watashikamana na dini yao kikamilifu na kusimamia misingi ya dini yao, kutavifanya vizazi vya sasa na vijavyo kuwa katika ustawi mzuri.

“Hatuwezi kuwa na jamii bora kama hatutojifunza dini yetu lakini pia viongozi wa dini jambo ambalo litawafanya waumini kuisimamia misingi ya dini ili jamii iwe na ustawi bora na kupunguza kwa kiasi kikubwa maswala yenye kudhoofisha Imani,” alisema ayoub.

Aidha alisema serikali ya mkoa wake imekuwa ikiunga mkono jitihada za dini zote za kuwaandaa waumini wao kwenye mambo ya kiimani jambo ambalo litaimarishwa Zaidi hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumzia masuala ya udhalilishaji katika jamii, alisema kuwa bado linaendelea, na seriklai ya mkoa wake imejipanga kulidhibiti na kuitaka jamii kuendelea kushirikian na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuvikomesha.

“Kwa bahati mbaya jambo hili limekuwa likihusishwa na baadhi ya viongozi wa dini, hatuwezi kukaa kimya na kuliacha liendelee hivyo nawataka wazazi, walezi na walimu kuwaelimisha watoto wetu madhara ya hivi vitendo,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Aidha alisema ipo haja elimu juu ya udhalilishaji ikaendelea kutolewa na kuwataka watoto kutoa taarifa mara wanapoona viashiria vya vitendo hivyo kwa wazazi au viongozi wao wa shehia ili hatua zichukuliwe.

Akizungumzia suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, Ayoub alisema wamejipanga vya kutosha kuhakikisha amani na utulivu inakuwepo kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Swala la kuwa na uchaguzi wa Amani, ndio kipaumbele chetu namba moja hivyo nawaomba viongozi wa dini kuhubiri na kuwahimiza waumini wenu juu ya amani mtakapokuwa katika nyumba za ibada kwani mna mchango mkubwa katika hili,” aliongeza Ayoub.

Baadhi ya waumini waliohudhuria hafla hiyo walisema mwaka mpya wa kiislamu unasheherekewa ikiwa ni sehemu ya kutekeleza sunna ili kuifanya jamii kutafakari matendo yao na kujipangia kwa ajili ya mwaka mpya.

Aidha walialiahidi kuendeleza mema na miongozo iliyoachiwa na kiongozi mkuu wa dini ya kiislamu Mtume Muhammad (S.A.W), pamoja na kuendeleza amani iliyopo kwa manufaa ya taifa.

Mwaka mpya wa kiislamu wa 1442 AH uliannza agosti 21 mwaka huu .