NA MWANDISHI WETU

KLABU ya Azam FC inakuja na tamasha kubwa la Azam FC Festival, kwa ajili ya kujiweka karibu na mashabiki hususani wakazi wa Chamazi inapotokea.

Uzinduzi wa wiki ya tamasha hilo ‘Wiki ya Chamazi’, unatarajia kufanyika leo Jumapili saa 4.00 asubuhi na kilele chake kitakuwa Agosti 23 .

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema kwamba tamasha la Azam FC Festival litakuwa la wiki moja kuanzia leo.

“Tumeandaa tamasha linaloitwa Azam FC Festival, tamasha hili ni maalumu kwa ajili ya klabu na mashabiki wake, hasa mashabiki waliopo Chamazi na mashabiki waliopo Temeke lakini na wengine wote kutoka sehemu yoyote ile ambayo wanaweza kufika katika eneo lile (Azam Complex).”

Baadhi ya mambo yatakayofanyika siku ya uzinduzi, ni mbio za vikundi vya Jogging vya eneo hilo, zitakazoanzia Mzambarauni hadi Mbande kabla ya kufanyika uzinduzi rasmi saa 4 asubuhi uwanjani Azam Complex.

Aidha kwenye uzinduzi huo kutakuwa na mashindano maalumu ya timu za waandishi wa habari za michezo, watakashindana kuwania ubingwa.

Wiki ya Chamazi itaendelea Jumatatu ijayo, kwa kuanza michuano rasmi ya wakazi wa Kata Chamazi, itakayohusisha timu tano za mitaa tisa ya kata hiyo dhidi ya nyingine zitakazoalikwa, michuano itakayohitimika siku ya kilele cha tamasha hilo kwa mchezo wa fainali.

Siku ya kileleni cha ‘Azam FC Festival’, Agosti 23 mwaka huu, mbali na kuwa na burudani kibao ndani ya viunga vya Azam Complex, pia timu hii itatumia siku hiyo kucheza mchezo rasmi wa kirafiki na timu moja ya nje ya nchi kwa ajili ya kutambulisha kikosi cha msimu ujao pamoja na jezi.

Vilevile kabla ya mechi hiyo kubwa, miongoni mwa mechi ya utangulizi, itakuwa ni ile fainali ya mashindano ya wakazi wa Chamazi pamoja na mechi za timu za vijana za Azam FC.