SMZ yafungua tena milango ya utalii

Wadau wa utalii wasema bado utalii haujachanganya

Kutokana na baadhi ya nchi za nje kutoruhusu safari za kitalii

NA HUSNA MOHAMMED

BAADA ya kupungua kwa ugonjwa wa corona hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Serikal ya Mapinduzi ya Zanzibar imeruhusu tena safari za ndege za kitalii kuwasili nchini.

Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mahmood Thabit Kombo, alisema serikali imefikia uwamuzi huo baada ya kujiridhisha na kiasi kidogo cha maambukizi ya corona.

Waziri Kombo alieleza pamoja na serikali kuruhusu shughuli za utalii kuendelea ni vyema shughuli hizo zikaendeshwa kwa kuzingatia tahadhari ya virusi vya corona kwa wageni kupimwa kila wanapoingia nchini, na wageni wote kutakiwa kuwa na bima zao za afya kabla hawajaingia nchini.

Takriban miezi tisa sasa dunia inaendelea kupambana na janga la corona lililozikumba nchi nyingi ulimwenguni ikiwemo Tanzania pale ugonjwa ulipoibuka kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana nchini China.

Aidha kwa hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ugonjwa huu ulianza mwezi wa Machi mwaka huu baada ya mgonjwa wa kwanza kupatikana.

MARADHI YA CORONA NA UTALII WA ZANZIBAR

Baada ya kuanza kwa maradhi hayo mwezi Machi mwaka huu serikali iliweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuzuia uingiaji wa ndege ambazo mara nyingi zimekuwa zikileta watalii ikiwa ni pamoja na kupambana na ugonjwa huo usiendelee kuambukiza nchini.

Kama nilivyoeleza hapo awali, hivi sasa serikali imeanza tena kuruhusu uingiaji wa ndege za kitalii ambapo kwa kuanzia ndege za shirika la ndege la Ethiopian Airlines, shirika la ndege la Qatar air na mengineyo.

Maeneo mengi ya kitalii yanaonekana kurudi kama awali ingawa kwa taratibu sana kufuatia baadhi ya nchi za Ulaya kutoruhusu ndege zao kufanya safari za kitalii.

KUWASILI KWA NDEGE ZA KITALII ZANZIBAR

Kwa kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeruhusu ndege za kitalii na kibiashara kuingia nchini shirika la ndege la Gulstrem kutoka Austria imeanza safari zake katika uwanja wa Abeid Aman Karume.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea wageni kutoka Austria, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Mulhat Yussuf Said, alisema, ndege hiyo ni ya kwanza kuingia nchini wageni walifuata masharti yote yaliyowekwa na serikali kabla ya kuingia nchini.

Alisema, katika ndege hiyo ilikuja na abiria kadhaa wakiwemo, watalii na waendesha ndege wawili ambapo wageni hao wataelekea katika hoteli za kitalii.

Aidha alisema kuja kwao wageni hao, kutaendeleza biashara ya utalii nchini ambapo takribani mienzi mitatu ilikuwa biashara hiyo imesitishwa kutokana na ugonjwa wa corona.

“Mwanzoni mwa Machi mwaka huu serikali ilipiga marufuku uingiaji wa ndege za kitalii na kibiashara baada ya kujitokeza mripuko wa janga la virusi vya corona ila imani yangu kwa sasa biashara ipo wazi na watalii wataendelea kuingia nchini” alisema.

Hivyo, aliwataka watalii kuingia nchini kupitia uwanja wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwani umezingatia usalama kwa watalii wanaoingia nchini.

Aidha alifamaisha kuwa wageni walioingia nchini awali walipimwa joto la mwili na kupakwa dawa wakati wakishuka katika ndege na baadae kuendelea na utaratibu uliokuwepo.

Sambamba na ndege hiyo, lakini shirika a ndege la Ethiopian airlines nalo pia linaleta huduma za usafiri Zanzibar na kwamba watalii na abiria kutoka nje wanawasili Zanzibar kipindi hiki cha kupungua ugonjwa wa corona.

Pia shirika la ndege la Qatar nalo limeanza kuleta watalii pamoja na wageni wakati huu wa kupungua kwa ugonjwa wa corona Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

BALOZI WA ITALIA AZUNGUMZA NA WAZIRI MWENYE DHAMANA YA UTALII ZANZIBAR

Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni ameipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zilizochukuliwa ili kudhibti ugonjwa wa corona na kufungua tena milango ya utalii nchini.

“Nimetembelea maeneo mbalimbali ya kitalii ikiwemo mahoteli, sehemu za fukwe na baadhi ya vituo vya afya ili kuhakikisha usalama wa raia wetu watakao kuja Zanzibar unazingatiwa”, alisema Balozi.

Alisema Zanzibar ni kituo muhimu cha kiutalii kwa raia wa Italia. hivyo amekuja kukagua na kuhakikisha kwamba raia wao wanakuwa salama wapoingia Zanzibar, jambo ambalo amekubaliana nalo.

Nae Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, alimuhakikishia Balozi wa Italia nchini Tanzania usalama wa raia wake wawapo Zanzibar kwa shughuli za kitalii.

Akizungumza na Balozi huyo ofisi kwake Kikwajuni Zanzibar, takriban wiki tatu sasa, alisema Italia ni mdau mkuu wa kuleta watalii ukilinganisha na mataifa mengine ya Ulaya kutokana na uwekezaji mkubwa waliofanya nchini.

Alisema lengo kuu ni kurejesha soko la watalii wa Italia Zanzibar ni baada kufunguliwa milango ya utalii visiwani hapa ili kuinua uchumi wa Zanzibar ambao umeathiriwa vibaya na maradhi ya corona.

“Tumefanya majadiliano na Balozi huyu kuhusu namna ya kuresha tena wageni wao kuja Zanzibar ikwemo namna ya kurejesha ndege za kitalii na kuja kujionea hali halisi ya usalama wa maeneo ya kitalii ilivyo Zanzibar”. alisema Waziri

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya kale Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo, akisisistiza kwa waandishi wa habari alipotembelewa na Balozi wa Italia, Robert Mangoni, huko ukumbi wa Wizara ya habari Kikwajuni Zanzibar.

Aidha alifafanua kuwa bado utaratibu wa kuwapima afya bado unaendela na yeyote atakegundulika na dalili za corona taratibu za afya zitafuata ili kuwaweka salama wananchi dhidi ya ugonjwa huo.

WAFANYABIASHARA WA KITALII WANAZUNGUMZAJE

Fatma Mwalimu ambae kazi yake ni kuuza batiki, kusuka nywele na kuwachora piko watalii katika eneo la Ngome kongwe ndani ya Mji mkongwe, alisema ingawa serikali imefungua utalii lakini bado utalii haujachanganya vyema.

“Tuna matumaini kuwa mwisho wa mwezi huu na Septemba biashara inaweza kuchanganya lakini kwa sasa bado”, alisema.

Nae Dereva wa gari za kubeba watalii ya Private hire, Said Abbas, alisema amekuwa akipata oda ya wageni wachache jambo linaloonesha bado utalii haujachanganya licha ya wakati wa msimu wa utalii kwa sasa.

“Kipindi kama hiki unapata oda ya watalii muda wote, lakini kwa sasa kidogo tu unapata na siku nyengine hupati kabisa.

WAFANYAKAZI WA MAHOTELI YA KITALII WANAZUNGUMZIAJE

Juma Ali anaefanya kazi katika hoteli moja ya kitalii Michamvi, yeye alisema kazi katika hoteli hiyo kwa sasa imefungwa na tangu kusitishwa kuja kwa ndege za kitalii bado hawajaanza kazi.

“Utalii uliporuhusiwa na ndege kuruhusiwa kuja Zanzibar tulifurahi sana, lakini mabosi wetu walitupigia simu tusubiri kwanza hadi mwezi wa Septemba”, alisema.

Nae meneja wa hoteli moja ya kitalii katika mji mkongwe wa Zanzibar ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema wamepata oda mwezi wa Septemba kupokea watalii wan chi mbalimbali ikiwemo Italia.

“Unajua baadhi ya nchi bado hawajafungua milango ya utalii hasa ndege zao kufanya safari nchi nyengine na ndio maana bado utalii wetu haujachanganya, lakini tuna Imani mwezi huu mwisho na mwezi ujao biashara itachanganya”, alisema.

KATIBU MTENDAJI KAMISHENI YA UTALII

Katibu Mtendaji kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Abdullah Mohammed alisema sekta ya utalii imepata athari katika kipindi cha maradhi ya corona hali ambayo ilipelekea uchumi wa nchi kupungua kwa asilimia tatu.

Alisema, hali imejitokeza kutokana na wananchi wengi wa Zanzibar kutoitilia mkazo dhana ya utalii kwa wote ambayo ndio dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kutegemea zaidi watalii kutoka nje.

Alisema pia corona imeonesha wazanzibari kuwa sio kitu ambacho wanachokiona ikiwemo wazungu wanaokaa mahoteli, wanaokuja kupitia viwanja wa ndege na bandarini pia hata gari zinazobeba abiria zinategemea sekta ya utalii.

Aidha, anabainisha kwamba, utalii ni sekta inayoengwa engwa na kuendelea kutegemewa lakini ni lazima wazanzibari wafahamu kwamba utalii wa ndani ni muhimu sana.

Hata hivyo, alisema baada ya kuwepo kwa maradhi hayo wananchi hasa waliokuwepo kwenye mnyororo wa uchumi ikiwemo wafanyabishara, wakulima, wachuuzi na watu wengine wamefahamu lengo la Rais kwa kufanya utalii wa ndani na kuwekeza wenyewe kwa kufanya utalii wa ndani kwa kutembea katika vivutio vyao.

“Kwa mfano China inategemea sana utalii wa ndani kuliko watalii wa kimataifa wanaokwenda nchini humo kutoka nchi mbalimbali na wanatosheleza kabisa kufanya soko la utalii na biashara zao zinakwenda,” anasema.

Alisema Zanzibar ni tajiri kwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii kwani mpaka sasa kisiwani Pemba ina zaidi ya vivutio 80 vya utalii na Unguja zaidi ya 100.

“Tungekuwa tunafanya utalii wa ndani na kujipanga kufanya utalii basi tungezuia wageni wasije nchini kwa sababu ya maradhi na ingekuwa corona haijaja kwetu basi wenyewe ingekuwa tunaendelea hapa hapa,” anasema.

Dk. Abdulla, aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar wasitegemee wageni pekee na badala yake kubuni biashara nyengine na hata kuchora picha ambazo zinaendana na wazanzibari katika utalii wa ndani.

Hata hivyo, anaimani kuwa nchi za nje zitakapofungua milango yake ya utalii na kuruhusu ndege kuja hasa kwa kuwa balozi wa Italia ameona hali halisi ya utalii Zanzibar kwa ziara yake ya karibuni, ni wazi kuwa utalii utarudi tena kwa nguvu.

Nae Maulidi Yussuf, ambae ni Mkurugenzi wa Zanzibar Youth Forum (ZYF), aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kitalii ikiwa ni pamoja na kujishughulisha na biashara ndogondogo.

“Kama tunavyojua corona bado ipo haijesha imepungua tu, milango ya utalii imeshafunguliwa, vijana msikae nyumanyuma utalii upo hata kipindi cha corona seuze sasa ugonjwa imepungua”, alisema.

HALI HALISI YA UTALII ZANZIBAR KABLA YA CORONA

WATALII wakiwa katika mtaa wa Shangani Zanzibar wakiangalia vitu vya kitalii katika maduka ya mtaa huo wakati wakiwa katika matembezi yao katika mitaa ya kihistoria ya Zanzibar.

Kabla ya ugonjwa huo kuingia duniani idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 376,242 mwaka 2016 hadi watalii 433,474 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 28.

Aidha Machi mwaka huu idadi ya watalii ingeongezeka na kufikia 800,000 lakini kutokana na janga hilo mwezi huo jumla ya watalii 20,584 ambapo mwezi Machi mwaka jana ni watalii 33,883 walioingia.

Hata hivyo, mwezi wa April mwaka huu, Zanzibar imepata athari ya kutoingia watalii na kutegemea utalii wa wageni kwani ilipokea wageni wasiozidi 300 wakati mwaka jana katika kipindi hicho walipokea wageni zaidi ya 2000.

Kuhusu idadi ya watalii kupanda kabla ya kuibuka kwa janga hilo, sera na mikakati ya serikali iliwataka watendaji waliyopewa majukumu ya kuutangaza utalii kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Imefika wakati wananchi kujifunza kupitia janga hilo na kutilia manani maneno ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein kuwasisitiza wazanzibari kuthamini vitu vya kwao hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhamasisha utalii wa ndani.

Sekta ya utalii ni sekta inayochangia sana katika uchumi wa nchi hasa hapa Zanzibar ukiachilia zao la karafuu huku uchumi huo ukikuwa kwa wastani wa zaidi ya asilimia 7.

Utalii pia kwa Zanzibar unachangia pato la taifa kwa asilimia 27 na zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni zinapatikana kutokana na watalii wengi kupenda mandhari ya Zanzibar na utamaduni wake ambao una thamani huvutia takriban zaidi ya watalii 500,000 kwa mwaka.

Mapato hayo yanapatikana kwa watalii wenyewe kupitia viwanja vya ndege, bandarini, watembeza watalii sehemu mbalimbali ikiwemo katika mashamba ya viungo na maeneo mengine.

Hivyo, ni wazi kuwa baada ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa sasa kufungua milango wazi baada ya kupungua corona, tuna Imani kwamba utalii utarudi tena kama awali.