Mchakato wa wawakilishi kumalizwa Kisiwandui

Majina kupitishwa kwenye kamati mbili

NA KHAMISUU ABDALLAH

BAADA ya vikao vya ngazi ya juu vya Chama cha Mapinduzi (CCM), vilivyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni kupitisha wagombea ubunge kwa chama hicho, hatima ya wawania ujumbe wa Baraza la Wawakilishi iko mikononi mwa vikao vitakavyofanyika baadae hapa Zanzibar.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alieleza hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo, kufuatia watu wengi visiwani hapa kutaka kujua hatima ya wawania uwakilishi baada ya wabunge kupitishwa mjini Dodoma.

Katibu huyo alibainisha kuwa kamati zitakazokaa katika vikao hivyo na kupitisha wagombea walioomba kuteuliwa nafasi ya uwakilishi kwa tiketi ya CCM ni kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar na sekretarieti.

Catherine alibainisha kuwa bado haijafahamika tarehe ya kufanyika vikao hivyo, vitakavyoamua wanaCCM watakaosimama kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wanaCCM na wananchi kuwa watulivu na kwamba chama kitatekeleza jukumu hilo na hatimaye kuwapata wogombea watakaopeperusha bendera kwenye uchaguzi huo.

Hivi karibuni halmashauri kuu ya taifa chini ya Mwenyekiti wa CCM Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ilipitisha majina ya wagombea wa nafasi ya ubunge katika majimbo mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa majimbo ya Pemba waliotangazwa ni Abdalla Rashid Othman Jimbo la Pandani, Juma Shaaban Juma jimbo la Wete, Ramadhan S Ramadhan jimbo la Chake Chake, Juma M. Juma jimbo la Chonga, Juma H. Omar jimbo la Ole na Khamis K. Ali jimbo la Wawi.

Wengine ni Ahmed Juma Ngwali jimbo la Ziwani, Mohammed A. Mwinyi jimbo la Chambani, Rashid Ali Rashid jimbo la Kiwani, Khamis S. Suleiman Jimbo la Mtambile na Proffesa Makame Mbarawa jimbo la Mkoani.

Majimbo ya Unguja ni Juma Usonge Hamad jimbo la Chaani, Yahya A. Khamis jimbo la Kijini, Khamis A. Vuai jimbo la Mkwajuni, Simai H. Saadik jimbo la Nungwi, Juma O. Hija jimbo la Tumbatu na Mbarouk J. Khatib jimbo la Bumbwini.

Wengine ni Soud M. Juma jimbo la Donge, Abdullah Ali Hassan jimbo la Mahonda, Haji Makame Mlenge jimbo la Chwaka, Khalifa Said Suleiman jimbo la Tunguu, Khamis Chilo jimbo la Uzini, Ravia Idarous Faina jimbo la Makunduchi, Jaffar Sanya Jussa jimbo la Paje na Mustafa Mwinyikondo jimbo la Dimani.

Aidha wengine ni Abass Ali Hassan jimbo la Fuoni, Mohammed Ali Jimbo la Kiembesamaki, Kassim H. Haji jimbo la Mwanakwerekwe, Haji Amour Haji jimbo la Pangawe, Mwantakaje Juma jimbo la Bububu, Zubeida Kh. Shaibu jimbo la Mfenesini, Abdulghafar Idrisa jimbo la Mtoni na Zahor M. Haji jimbo la Mwera.

Waliteuliwa wengine ni Maulid Saleh Ali jimbo la Welezo, Mussa H. Mussa jimbo la Amani, Ussi Salum Pondeza jimbo la Chumbuni, Mwanakhamis Said jimbo la Magomeni, Salum Hassan Abdullah Turkey jimbo la Mpendae.

Wengine ni Ali Juma Mohammed jimbo la Shaurimoyo, Ali Hassan King jimbo la Jangombe, Hamad Masauni Yussuf jimbo la Kikwajuni, Ahmada Yahya Abdulwakil jimbo la Kwahani na Mohammed S. Omar jimbo la Malindi.