NA TATU MAKAME
WAFANYABIASHARA na wajasiriamali wanawake wametakiwa kutumia umoja wao kutumia fursa zinazojitokeza kujiendeleza kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake zanzibar (ZWCC).


Mkutano huo ulioambatana na uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo, ulifanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo katika jengo la Mamlaka ya Udhibiti wa nishati na maji (ZURA), Maisara mjini Zanzibar.


Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Dira ya Maendeleo ya 2020 ilidhamiria kufikia uchumi wa kati kwa kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii ya watu wa Zanzibar.
Alisema mikakati ya serikali kufikia malengo hayo ifikapo mwaka 2020 imetafsiriwa kwenye mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA III) jambo ambalo limefikiwa.


“Mkakati huo una dhamira ya kukuza matokeo ya kiuchumi na kufikia lengo kwa wananchi wote wa Zanzibar ili kuondokana na umaskini uliokithiri,kwa kupata huduma bora za kijamii kwa kuishi katika mazingira mazuri,” alieleza Balozi Amina.


Aidha Balozi Amina alisema ili wanawake waweze kufikia malengo hayo ni lazima wawe na uthubutu katika kuleta ukuaji wa uchumi wenye fursa sawa kwa vijana, wanawake na wanaume.
Aliongeza kuwa ni matumaini yake kuwa malengo hayo yataendelezwa na serikali ijayo hivyo jumuiya hiyo inapaswa kuweka misingi imara itakayowawezesha kunufaika nayo.


“Mgombea wa urais wa CCM (Chama Cha mapinduzi) DK. Hussein Ali Mwinyi, miongoni mwa malengo yake, ameahidi kuboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa kipaumbele wanawake kama yalivyo makundi mengine,” aliongeza Balozi Amina.


Balozi huyo alifahamisha kuwa taasisi binafsi, imeweka sera elekezi zinazohimiza kujenga mashirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi katika kuharakisha maendeleo.


Alieleza kuwa amefuatilia kwa karibu mchakato wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo na kuridhishwa juu ya utendaji wa kuanzisha kwa haraka na kuishukuru mamlaka ya uendelezaji viwanda vidogovidogo na vya kati (SMIDA), taaisisi ya viwango Zanzibar (ZBS) na shirika la taifa la biasahara (ZSTC) kwa msaada walioutowa ukiipa jumuiya kuhakikisha wazo hili linasimama.
Aliwataka wanawake pale wanapoamua kufanya jambo kuweka amri na kuandaa mbinu halali za biashara kupitia elimu tofauti ambazo zinatolewa na zitakazotolewa na jumuiya hiyo.


Awali katibu wa muda wa jumuiya hiyo Fatma Mabrouk Khamis alieleza kuwa licha ya kufanikiwa kujenga umoja bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za utamaduni.
“Jamii yetu bado inawaona wanawake viumbe dhaifu,kutoshirikishwa katika ngazi za maamuzi pia wanawake wenyewe kujilemaza,” alisema Fatma.


Alieleza kuwa malengo ya jumuiya hiyo ni kuwaendeleza kielimu kwa kuwapatia mbinu mbali mbali za kibiashara ili wawe na tija na kuondoa urasimu katika biashara.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama zaidi ya 200 kutoka Unguja na Pemba, Fatma Khamis Mabrouk alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Fatma Hasan akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti huku Asha Abdulkheir Mohammed, Msimu Mwinyi Ramadhan, Fatma Abas Mohammed, Naima Mwenzagu, Zeyana Ahmed Kassim na Mvita Mustafa Ali kuwa wajumbe wa bodi.