NA WAANDISHI WETU, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza taasisi zinazosimamia ujenzi wa miundombinu, manispaa, mazingira na serikali ya Mkoa Mjini Magharibi, kuitafutia ufumbuzi changamoto ya mmong’onyoko katika fukwe za bahari.
Balozi Seif alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara fupi ya kuangalia eneo la fukwe ya Mazizini ambalo limeathirika vibaya kutokana na kupanda kwa kina cha maji ya bahari na kusababisha barabara iliyopita pembezoni mwa eneo hilo kumong’onyoka.
Alisema zipo athari nyingi zilizojitokeza za uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, huku akiyataja maeneo ya Msuka na Mazizini kama mfano wa athari za wazi za mmong’onyoko unaosababisha ya nguvu za maji ya bahari.
Alisema jamii inashuhudia athari za mazingira ambapo pamoja na kwamba kuna tatizo la mabadiliko ya tabianchi, lakini katika baadhi ya maeneo wananchi wanahusika kwa kiasi kikubwa kwenye uharibifu wa mazingira
Makamu wa Pili, aliwaeleza viongozi na wataalamu katika taasisi hizo kuelewa kwamba wana jukumu walilopewa na ndio wenye dhima ya kuhakikisha uharibifu wa mazingira unadhibitiwa sambamba na kuzuia mmong’onyoko katika maeneo ya fukwe.
Awali mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema serikali kupitia wizara hiyo imeshatiliana saini mkataba na kampuni ya China inayojenga barabara ya Bububu hadi Mkokotoni kwa ajili ya ujenzi wa miradi mitatu hapa nchini.
Mustafa alimueleza Balozi Seif miradi hiyo ni pamoja na mtaro wa maji machafu wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Daraja la Upenja kuelekea Kiwengwa na ujenzi wa ukuta wa kuzuia maji ya bahari utakaolindwa na mawe makubwa pembezoni ya ufukwe wa Mazizini.
Alisema mradi huo wa ukuta utakwenda sambamba na bomba la kupitishia maji machafu na ya mvua yanayotiririka kuingia pwani ya Mazizini ili kuzuia mmong’onyoko wa ardhi kwa mujibu wa ushauri wa wataalamu wa taasisi za Mazingira.
Naye kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja alisema katika kufanikisha suala hilo ipo haja ya kuwepo kwa timu maalum itakayopewa jukumu la kulinda eneo hilo kwa hatua ya kwanza ili kuzuia uvamizi wa kimazingira unaoweza kuharibu azma ya uiimarishaji wa eneo hilo.
Mjaja alisema kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuathiri sehemu mbali mbali za dunia ni vyema miradi inayoanzishwa ya kunusuru mmong’onyoko wa ardhi ikalenga kudumu kwa kipindi kirefu ili kupunguza gharama kubwa.