NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
LICHA ya kutokuwepo kwa mgonjwa au mtu anaehisiwa kuwa na virusi vya covid 19 nchini, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema jamii inapaswa kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo.
Alisema maradhi hayo yameleta hofu na simanzi duniani hali iliyopelekea baadhi ya mila na taratibu za Wanaadamu kama vile kupeana mikono kuachwa kwa muda ili kuepuka maambukizi ya janga hilo thakili.
Balozi Seif alisema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya kinga dhidi ya virusi vya corona kwa matumizi ya walimu na wanafunzi wa skuli 12 zilizomo ndani ya jimbo la Mahonda iliyofanyika katika skuli ya sekondari Kitope.
Balozi Seif ambae ni Mwakilishi anaemaliza muda wake katika jimbo hilo, alieleza jamii inapaswa kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona na bado itakuwa ni suala la lazima katika kipindi hiki cha mpito kwa vile maradhi hayo yanaendelea kuitesa dunia katika baadhi ya mataifa ya Afrika.
Alisema serikali ililazimika kupunguza masharti yaliyoainishwa awali kupunguza maambukizi ya virusi hivyo baada ya jihitada kubwa zilizochukuliwa na serikali, wadau wa sekta ya afya na wananchi pamoja na taasisi za kitaifa na zile za kimataifa.
“Hatua za kunawa mikono kwa maji ya kutiririka, vitakasa mikono na uvaaji wa barakoa (maski) katika maeneo yenye misongamano ni vyema ikaendelea kuzingatiwa na kufanywa kama suala la kawaida katika jamii yetu,” alisisitiza Balozi Seif.
Aidha Balozi Seif aliwashukuru na kuwapongeza wananchi nchini kwa kuwa wasikivu na kufuata maelekezo ya serikali kuu na wataalamu wa afya jambo lililopelekea taifa kubaki salama.
“Tuna mfano wa majirani zetu wa mataifa ya Madagascar na Botswana waliofanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona na kuamua kulegeza vikwazo kwa hatua kubwa ambayo sasa inawagharimu kutokana na kurejea kwa kasi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo,” aliongeza.
Alisisitiza umuhimu wa wanafunzi na walimu maskulini kuvitumia vifaa vya kinga kutokana na maeneo yao makubwa kuendelea kuwa na msongamano mkubwa wa watu.
Aliwaomba wananchi hao kwa vile yeye anapumzika utumishi wa jimbo washirikiane na viongozi wapya wa jimbo la Mahonda.
Mapema Katibu Tawala wa wilaya ya Kaskazini ‘B’ Makame Machano Haji kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Rajab Ali Rajab alimshukuru Balozi Seif kwa kukamilisha ahadi alizotoa wakati wa utumishi wake kwa jimbo hilo utakaokamilika hivi karibuni.
Makame alisema uongozi wa wilaya hiyo umejitolea kubeba dhima ya kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinasimamiwa kwa faida na maendeleo ya wananchi wote.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Walimu Wakuu wa skuli zilizokabidhiwa vifaa hivyo, Mwalimu Mkuu wa skuli ya sekondari Kitope mwalimu Simai Haji Hamad alisema kama wasimamizi wa wanafunzi wa skuli hizo wako tayari kuona vifaa walivyokabidhiwa vinatumika kwa lengo lililokusudiwa.
Mwalimu Simai alimuomba Balozi Seif kutokuwa mbali na wadau wa elimu wa jimbo hilo kwa kuendelea kuwashauri kila atakapohitajika kufanya hivyo ili ile kiu ya wananchi wa jimbo hilo ifikiwe.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais alikabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni 44 ikiwa ni pamoja na sabuni, ndoo, vitakasa mikono pamoja na maski.