NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wahandishi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kupeleka serikalini mahitaji ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa maradi wa maji katika mtaa mpya wa Pagali.
Balozi Seif alieleza hayo alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, katika mtaa wa Pagali uliopo Chake Chake.
Aliwaeleza wahandisi hao wanatakiwa kuharakisha kazi ya upelekaji maji katika mtaa huo na kama kuna changamoto wanapaswa kuiarifu serikali ili mradi huo umalizike kwa wakati.
Makamu huyo alisema itapendeza vifaa vinavyotumika katika mradi huo vinakuwa na ubora unaokubalika ambavyo vitadumu kwa kipindi kirefu hali itakayotoa uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo katika mtaa huu.
Alisema kwa muda mrefu kwenye miradi ya maji safi kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wahandisi waliopewa jukumu la kusimamia kazi hununua vifaa vilivyo chini ya kiwango.
Alisema baada ya muda kwa sababu vifaa vilivyowekwa ni vya kiwango cha chini husababisha wananchi kupata usumbufu kwa kujitokeza matatizo ya kukatika kwa maji mara kwa mara.
Awali mkurugenzi mkuu wa wakala wa majengo Zanzibar, Ramadhan Mussa Bakari alisema wajenzi wa mradi huo kwa sasa wanasubiri kukamilika uwekaji wa miundombinu ya bustani ili wakamilishe kazi ndogo ndogo zilizobakia.
Ramadhan alimueleza Balozi Seif kwamba matengenezo yaliyobakia katika kipindi hichi yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na makabidhiano ya mradi yafanyika mwishoni mwa mwezi.
Alisema kinachozingatiwa ni jinsi ya kuwapata washauri na wataalamu wa masuala ya miti na bustani kutoka taasisi ya misitu pamoja na manispaa, ili bustani itakayooteshwa ilingane na hadhi ya nyumba za viongozi wakuu.
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mtaa wa Pagali uliopo mjini Chake Chake ulianza mnamo mwezi Juni mwaka 2018.