Asema utasaidia kuinua sekta ya utalii

NA WAANDISHI WETU, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kuandaa mpango wa muda mrefu utakaozingatia mahitaji ya maeneo ya kazi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Balozi Seif alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigunda uliopo mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo ndege ndogo zina uwezo wa kuruka na kutua.

Alisema endapo watazingatia kuwa na mpango huo, utasaidia kupunguza gharama za fidia kwa mali za wananchi na utatoa fursa kwa Mamlaka kujipangia mipango yao kwa mujibu wa muongozo na vigezo vya kimataifa.

Alisema yapo matukio kadhaa yanayoendelea kushuhudiwa ambapo serikali hulazimika kulipa fidia kutokana na miradi inayotekelezwa na taasisi za umma baada ya maeneo yanayoanzishwa miradi hiyo kuwa chini ya milki za wananchi.

Balozi Seif aliutaka uongozi wa Mamlaka hiyo ya Viwanja vya Ndege, kuhakikisha kwamba kazi hiyo wanaitekeleza kabla baadhi ya watu kuvamia maeneo hayo baada ya kuanza kwa harakati za uwanja huo.

Aliupongeza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar kwa jitihada zao za kusimamia ujenzi wa uwanja huo na kushauri harakati zao ni vyema zikaenda sambamba na kujengewa uzio utakaoepusha uingiaji wa kiholela kwenye eneo hilo.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhia kujengwa kwa uwanja huo kutokana na mabadiliko makubwa ya mwenendo mzima wa shughuli za utalii, biashara na mawasiliano ya usafiri wa anga kati ya Zanzibar, mikoa ya Tanzania bara.

Balozi Seif alibainisha kwamba watalii waliopanga kutembelea ukanda wa Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja wanaweza kwenda moja kwa moja kwa kutumia ndege kutoka maeneo tofauti badala ya usafiri wa gari.

“Kwa vile uwanja huo utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege zitakazobeba abiria zaidi ya 70 utasaidia kupunguza msongamano katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume”, alisema Balozi Seif.

Aliushauri Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kufikiria uwezekano wa kuwepo kwa kiwanja cha Ndege katika ukanda wa Kusini mwa Kisiwa cha Unguja kwa lengo la kuimarisha huduma za kiuchumi.

Awali msimamizi wa Ujenzi wa Uwanja huo wa Ndege wa Kigunda, Mhandisi George alisema kazi zinazoendelea uwanjani hapo kwa sasa ni ukamilishaji wa uwekaji wa kifusi kwa tabaka la mwisho.

George alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua ya utandikaji wa lami kwenye uwanja huo inatarajiwa kuanza Mwezi wa Oktoba mwaka huu ukiwa na urefu wa kilomita mbili zitakazowezesha kutua na kuruka kwa ndege tofauti zikiwemo aina ya ‘Fokker’.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Said Iddi Ndumbogani alisema ujenzi wa uwanja wa Kigunda ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

Ndumbogani alisema mradi huo utahitaji kuwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 400 zitakazofanana na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ambao utawezesha ndege kubwa za aina yoyote kuweza kuruka au kutua bila ya mashaka.

Matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigunda yalianza mwishoni mwa mwaka 2019 ambapo jiwe la msingi la kuanza ujenzi huo liliwekwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.