NA OTHMAN KHAMIS

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema wananchi wanapaswa kuzingatia matumizi bora ya miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na serikali.

Balozi Seif alieleza hayo jana wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara nne zinazojengwa kwa kiwango cha lami chini ya usimamizi wa Mfuko wa Barabara kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu inayosimamia Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika (BADEA).

Barabara hizo ni pamoja na Kinduni –  Kitope yenye urefu wa kilomita nne, Mwera – Mambosasa hadi Mashine ya Maji Meli tano yenye urefu wa kilomita 3.4, Fuoni Polisi hadi Kibonde Mzungu kilomita 1.2 na Jumbi hadi Koani yenye urefu wa kilomita 6.3.

Balozi Seif alielezea kuridhika na kazi nzuri inayofanywa na wahandisi wazalendo ya ujenzi wa barabara hizo jambo ambalo litaleta faraja kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein wakati atakapo staafu.

Aliwashauri wahandisi hao watakapokabidhiwa jukumu la ujenzi wa barabara wahakikishe wanazingatia mbinu za kisasa hasa kutokana na uhaba wa rasilimali ya mchanga inayovikabili visiwa vya Zanzibar.

“Wahandisi na wananchi lazima waelewe kwamba Zanzibar kwa sasa ina upungufu mkubwa wa mchanga, hivyo katika miradi wanayoianzisha  ni vyema wakazingatia changamoto hiyo ili wasije kwama katika kazi zao”,alisema Balozi Seif.

Balozi Seif aliishauri wizara inayosimamia masuala ya ujenzi na fedha kuhakikisha kwamba suala la malipo linafanyika kabla ya kukabidhiwa miradi husika kwani haitopendeza kuona mradi ushakabidhiwa lakini bado kuna deni.

Balozi Seif alitoa onyo kwa vijana wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi kuacha mara moja tabia isiyostahiki kwa mila na utamaduni wa asili kwani unagharimu maisha ya wananchi.

Alibainisha kwamba uimarishaji wa miundombinu unaofanywa kwa kushirikiana na wahisani, mataifa rafiki na taasisi za kimataifa unazingatia zaidi na kwa kina kuwarahisishia usafiri wananchi wake katika harakati zao za kujitafutia riziki.