NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amepongeza ushirikiano wa karibu uliopo kati ya wizara zinazosimamia sekta ya nishati na madini nchini Tanzania, baina ya Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Balozi Seif alisema hayo kwenye makaazi yake yaliyopo mtaa wa Farahani jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waziri anayesimamia wizara ya Nishati na Madini wa serikali ya Jamhuri ya Muungano, Dk. Medard Kalemani.

Makamu huyo alisema kasi ya uwekezaji hasa kwenye ujenzi wa viwanda, biashara, utalii na ujenzi wa miji mipya ya kisasa kunahitajika pawepo uhakika wa nishati ya umeme.

Alisema nchi imepiga hatua kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu katika sekta ya viwanda bara na Zanzibar ambapo kuna ulazima wa wanaosimamia wahakikishe uwekezaji huo unaofanywa unawanufaisha vijana katika suala zima la ajira.

Balozi Seif alisema kwamba wapo vijana wengi wanaomaliza masomo vyuo vikuu na elimu ya sekondari wanaohitaji ajira ili kuendesha maisha yao, ambapo njia pekee kwa sasa ya kukabiliana na tatizo la ajira ni kuimarika kwa sekta ya viwanda.

Balozi Seif aliishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya Nishati kwa uamuzi wake wa kusamehe madeni yaliyokuwa yakilidai Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Makamu wa Pili aliuomba uongozi wa wizara ya Nishati na Madini na ule wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuendelea kulipatia msaada Shirika la Umeme Zanzibar, ili kuona huduma za nishati ya umeme zinamfikia kila muhitaji.

Awali waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Medard Kalemani alisema wizara hiyo kupitia shirika la Umeme Tanzania wakati wote huhakikisha kuwa huduma ya umeme inapatikana wakati wote katika maeneo yote Tanzania bara na Zanzibar.