NA HANIFA SALIM

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzaibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema, ustawi wa sekta ya kilimo unahitaji amani na utulivu ili wananchi wanaotegemea sekta hiyo wapate maendeleo.

Alisema, bila ya amani na utulivu hakuna mwananchi atakaethubutu kwenda shamba, baharini au msituni kutafuta riziki.

Alisema hayo wakati akiyafunga maonyesho ya tatu ya kilimo yaliyofanyika katika uwanja wa maonesho Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema, haikamiliki kujivunia kwamba taifa limesheheni amani bila ya maendeleo endelevu katika sekta zote ikiwemo kilimo.

Aliipongeza  Wizara  ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa  kusimamia na hatimae kufanikisha  maonyesho hayo.

Alisema umahiri wa wizara hiyo umepelekea wananchi wengi kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo sambamba na kupata fursa ya kuuza bidhaa zao.

Alibainisha kwamba vijana wajasiriamali wakiwemo wanawake wamejifunza mambo mengi ya kukuza mitaji yao.

Alisema mambo hayo yanatimiza dhamira ya wizara ya kilimo, kuwa maonyesho ya kilimo ni njia moja wapo ya kuwafikia wananchi kwa muda mfupi.

Kuhusu uchaguzi mkuu, alisema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anatumia haki yake ya kidemokrasia bila ya kushawishiwa kuchagua kiongozi amtakae pamoja na kulinda amani iliyopo.

Alisema, maisha bado yataendelea kuwepo baada ya uchaguzi,  hivyo uchaguzi usiwe sababu ya kuwagombanisha Watanzania.

“Tuwe watii wa sheria za nchi ipasavyo katika kipindi chote cha uchaguzi kwani suala la kuilinda amani ya nchi hii ni jukumu letu sote,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk. Omar Ali Amir, alisema maonyesho hayo yamehudhuriwa na washiriki 189 kutoka taasisi na mashirika ya umma na binafsi kutoka Pemba, Unguja na Tanzania Bara.

Waziri wa wizara hiyo, Mmanga Mjengo Mjawiri alivishukuru vyombo vya ulinzi pamoja na  halmashauri kwa umakini wao uliosaidia kufanikisha  maonyesho hayo.

Ujumbe wa mwaka huu wa maonyesho ya tatu ya kilimo unasema ‘Tudumishe amani na utulivu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar’.