NA MARYAM HASSAN

MAFURUSHI saba ya bangi, yamempandisha katika mahakama ya mkoa Vuga mwanamama Johari Haji Mabula (28) mkaazi wa Mtule wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inaeleza kuwa, Mwanamama huyo alikamatwa maeneo ya sokoni Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Hati hiyo imesomwa na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Anuari Saaduni, mbele ya Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira.

Wakili huyo alidai kwamba, mshitakiwa alipatikana na dawa za kulevya mnamo Mach 9 mwaka huu majira ya saa 3:00 za asubuhi huko Mwanakwerekwe sokoni.

Alidai kuwa Johari alipatikana na mafurushi saba ya majani makavu yaliyokuwa yamezongwa katika magazeti akiwa ameyahifadhi kwenye ndoo, yakiwa na uzito wa gramu 900, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana jambo ambalo lilipingwa na wakili huyu, kwa madai kuwa kiwango alichopatikana nacho ni kikubwa.

Hivyo Hakimu Hamisuu aliahirisha shauri hilo na kuamuru mshitakiwa huyo kupelekwa rumande hadi Agosti 24 mwaka huu kesi yake itakapoanza kusikilizwa ushahidi, kwa sababu upelelezi umekamilika.