Chuo kinachowafunda wanawake kazi za mikono

Zipo za kuunga umeme wa jua, ufugaji nyuki na ushonaji

NA MWAJUMA JUMA

OGASTI 6 mwaka huu, kituo cha mafunzo ya utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua na kazi nyengine za mikono (Bare foot) kinatimiza miaka mitano huku kikiwa na mafanikio kadhaa ambayo yanabeba malengo halisi ya kituo hicho iliyojiwekea.

Kituo hicho kilichopo Kibokwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, kimeanzishwa kikiwa na lengo la kuwawezesha wanawake wasiosoma kiuchumi ili kujikimu kimaisha na familia zao.

Kituo hicho kikiwa kinatimiza miaka mitano kimefanikiwa kuwanufaisha akinamama 45 kwa kuwapa mafunzo ya utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua.

Akizungumza na Makala haya Pendo Yaride Sambayi, ambae ni mratibu wa kituo cha utengenezaji wa umeme wa jua, alisema jumla ya wanawake 13 walipatiwa mafunzo nchini India na 32 kituo cha Barefoot Zanzibar, ambapo kupitia wahitimu hao jumla ya nyumba 956 zimeunganishwa na umeme wa jua katika vijiji tisa vya Zanzibar.

Alivitaja vijiji vilivyounganishwa umeme kupitia kituo hicho kuwa ni pamoja na Matemwe, Bumbwini, Kandwi, Kinyasini, Makunduchi, Mtende na Mbuyutende kwa Unguja na Kisiwa Panza na Makoongwe kwa Pemba.

Aidha alisema wanafunzi 67 ambao kati yao sita walipata mafunzo ya ufugaji wa nyuki kutoka Tarakea Moshi katika kijiji cha Mbomaina Kikeleluwa ambao tayari wamehitimu masomo ya ufugaji wa nyuki, kutoka vijiji mbali mbali Unguja na Pemba ambao kwa sasa tayari mafunzo hayo wanayafanyia kazi.

Sambamba na hilo, lakini Pendo alisema vijana wengine 40 wamehitimu mafunzo ya kushona nguo za kawaida, nguo za wafugaji nyuki na saba wanaendelea na mafunzo, huku sita wakihitimu mafunzo ya utengenezaji wa taulo za kike (pads) na sasa wapo kituoni kwa ajili ya kuwasaidia mafundi ili kuongeza uzalishaji.