NA KHAMISUU ABDALLAH

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imefanya mabadiliko ya bei za mafuta zilizoanza kutumika rasmi jana.

Akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake Maisara, kaimu mkuu wa kitengo cha uhusiano, Khudhaimat Bakar Kheir, alisema mafuta ya petroli yatauzwa kwa shilingi 1,885 mwezi huu kutoka shilingi 1,751 ya mwezi uliopita tofauti ya shilingi 134 sawa na asilimia 7.6.

Aidha alisema mafuta ya dizeli yamepanda hadi shilingi 1,925 kwa lita kutoka shilingi 1,856 kwa lita kwa mwezi Julai tofauti ya shilingi 69 sawa na asilimia 3.7.

Kwa upande wa mafuta ya taa Khudhaimat, alisema bei ya reja reja ya mafuta ya taa kwa mwezi huu imeshuka na kufikia shilingi 1,188 kwa lita kutoka shilingi 1,800 kwa lita ya mwezi uliopita sawa na asilimia 34.

Akizungumzia mafuta ya meli (Banka), alisema kwa sasa ZURA haipangi pei za mafuta hayo kutokana na kutotumiwa na wananchi na badala yake kuwaachia wenyewe ikiwemo makampuni kama wanavyofanya Tanzania bara.

“Tumeona tusipange bei ya mafuta ya ndege, kwani mafuta haya hawatumii wananchi binafsi zaidi yanatumiwa na makampuni ya ndege makubwa,” alisema.

Alifahamisha kuwa sababu zilizochangia kupanda kwa bei za mafuta ya petroli na dizeli kwa mwezi huu kunatokana na kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia pamoja na soko la ndani kwa kupitia bandari ya Dar es Salam.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuwa bei zilizotangazwa na serikali ndio bei halali huku akitumia muda huo kuwasisitiza kununua mafuta katika vituo halali na kudai risiti pale wanapouziwa nishati hiyo ili kuepuka kuuziwa mafuta kimagendo au mafuta yasiyo salama kwa vyombo vyao.