NA MWANAJUMA MMANGA, ASIA MWALIM

KUTOKUWEPO kwa soko la kitalii kumeshababisha kushuka kwa bei za bidhaa  mbali mbali ikiwemo mboga mboga na matunda  katika masoko ya Zanzibar.

Wakizungumza na waandishi wetu wa Zanzibarleo wafanyabishara wa masoko mbali mbali wa Zanzibar  wamesema kushuka kwa bei hizo kunatokana na kufungwa kwa mahoteli ya kitalii kutokana na nchi nyingi kukumbwa na janga la Covid 19.

Wafanyabiashara hao wamesema hali ya soko hivi sasa limeshuka ukilinganisha na kipindi cha nyuma kwani baadhi ya bidhaa zilipanda bei na nyengine zilishuka kutokana na mahitaji yaliongezeka kwa baadhi ya nchi ikiwemo Kenya, kwa zao la Tangawizi na baadhi ya nchi mahitaji yalipungua kutokana na mardhi hayo.

Walisema bei ya tungule hivi sasa kilo shilingi 1000 ambapo bei ya nyuma ziliuzwa  kilo shilingi 3,500 hadi 3000, bei ya vitunguu maji kilo moja ilikuwa 10,000 hadi 7000 ambapo hivi sasa ni kilo shilingi 6000.

Bei ya Mbatata imerudi katika kiwango cha kawaida ambapo ilikuwa kilo shilingi 2000 hadi 1500, lakini hivi sasa imefika hadi 1000 hata kipindi cha skukuu,  bei ya Vitunguu saumu kilo shilingi 6000 na kipindi cha sikukuu ilikuwa shilingi 4,500 na hivi sasa ni shilingi 4,000.

“Vitunguu bei yake haipandi kiholela mara kwa mara kwa sababu matumizi yake sio makubwa ukilinganisha na Vitunguu maji au bidhaa nyengine’’alisema.