MINSK,BELARUS

BELARUS imethibitisha kifo cha kijana mmoja aliyekuwa anashikiliwa kizuizini kufuatia maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais nchini humo.

Kijana huyo alifariki dunia baada ya kuhamishwa gereza.

Kamati ya uchunguzi ilisema kwenye taarifa yake kwamba kijana huyo wa miaka 25 alifariki baada ya kukamatwa katika mji wa Gomel, kusini mashariki mwa nchi hiyo na kufungwa kwa siku kumi gerezani.

Wachunguzi hao walisema chanzo cha kifo bado hakijajulikana.

Kituo cha radio cha Free Europe kilimnukuu mama wa kijana huyo akisema mwanae alikuwa na matatizo ya moyo na alishikiliwa kwa muda mrefu kwenye gari ya polisi.

Kifo hiki cha karibuni kinaripotiwa wakati waandamanaji wa upinzani wakiandamana kupinga ukatili wa polisi.