UCHAGUZI wa rais nchini Marekani utakaofanyika Novemba 3 mwaka huu, umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu sana duniani kote kutokana sababu mbalimbali.

Miongoni mwa sababu hizo kwanza Marekani ni taifa kubwa duniani lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi, lakini kwa mataifa kama yetu yangependa kuona na kujifunza ukomavu wa demokrasia nchini.

Kwa wachumi zipo sababu za kiuchumi za kuufuatilia uchaguzi, lakini kwa mahasimu wa rais wa sasa Wamarekani Donald Trump nao wangependa kuona anavyokiacha kiti chake kilichopo ikulu ya ‘white house’.

Kwa hakina kinachoendelea hivi sasa nchini humo, ni kwa vyama vikubwa hasa democratic na republican kujipanga na kupanga safu kwa ajili ya kuelekea kampeni za kutafuta ushindi.

Katika moja ya jambo lililoshitua ulimwnegu lililofanywa na mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa Marekani, Joe Biden kutoka chama cha democratic, ni kumchagua mgombea mwenza mwanamke.

Hapo juzi, Biden alimthibitisha seneta Kamala Harris kutoka jimbo la California kuwa mgombea mwenza wake atakayesimama naye kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini humo.

Seneta Harris mwenye umri wa miaka 55 anakuwa mwanamke wa kwanza mweusi katika historia ya Marekani kugombea wadhifa huo.

Hakuna mwanamke aliyewahi kuwa rais au makamu wa rais nchini Marekani na kwamba ni wanawake wawili tu ambao wamewahi kuteuliwa na vyama vikuu vya Marekani kuwa wagombea wenza katika historia ya nchini.

Wanawake hao ni mdemokrat Geraldine Ferraro mwaka wa 1984 na Sarah Palin, wa chama cha republican, aliyeteuliwa na marehemu John McCain mwaka wa 2008, hata hivyo, hawakufanikiwa kushinda.

Kamala Harris ni nani?

Kamala Harris ni mama mwenye umri wa miaka 55, aliondoka kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais mwezi Disemaba mwaka jana baada ya kutofanikiwa kushinda katika mchuano wa uteuzi wa kiti cha urais wa chama cha democratic.

Alikabiliana kwa mara ya kwanza na Joe Biden wakati wa midahalo ya chaguzi za awali, ambapo alikosoa jinsi Biden alivyosifu mahusiano ya kiraia ya kikazi aliyokuwa nayo na seneta wa zamani ambaye alipendelea ubaguzi wa rangi.

Kamala Harris alizaliwa katika mji wa Oakland uliopo katika jimbo la California, ambaye anatokana na wazazi wahamiaji ambapo mama yake alikua ni muhindi kutoka barani Asia na baba yake mjamaica.

Seneta huyo ni mmoja wa watu mashuhuri sana ndani ya chama hicho, na alitajwa kama mmoja wa watu ambao wangeteuliwa kuwa wagombea-wenza wa Biden punde tu alipositisha kampeni yake ya kuwania uteuzi wa chama.

Alisoma hadi chuo kikuu cha Howard, ambacho ni moja ya vyuo maarufu walivyosomea watu weusi kihistoria ambapo aliwahi kueleza kuwa muda wake akiwa chuoni hapo umesaidia sana kujenga maisha yake.

Kamala alikua hasimu wa Biden katika mchakato wa ndani ya chama kuwania mchuano wa kuwania urais, hata hivyo kwa muda mrefu amekuwa amekuwa akichukuliwa kama mgombea wa nafasi ya pili baada ya Biden.

Mwanasheria huyo mkuu wa zamani wa California, amekua akitoa wito wa kufanyika kwa mageuzi katika polisi ya Marekani wakati wa maandamano ya kitaifa ya kupinga ubaguzi wa rangi.

Kamala mara kwa mara amekuwa akisema kuwa kwa wakati wote hujivunia utambulisho wake na hujieleza binafsi kama Mmarekani.

Mnamo mwaka 2019, Kamala aliliambia jarida la Washington Post kwamba wanasiasa hawapaswi kupewa nafasi kwasababu ya rangi au wanakotoka.

“Nilikua nataka kusema hivi, mimi ni mimi niliovyo. Nina uwezo. Unaweza kuhitaji kunielewa, lakini niko sawa na jinsi nilivyo”, alisema.

Pamoja na mitihani mingi ya kisiasa atakayokumbana nayo wakati huu wa kuelekea uchaguzi, hata hivyo atakuwa na kazi kubwa ya kupambana kwenye mdahalo na makamu wa rais wa sasa wa Marekani, Mike Pence utaakofanyika Oktoba 7 mwaka huu huko Salt Lake City, Utah.

Katika maeleo yake Biden alimuelezea Kamala kama mwanamama mpiganaji  asiye na uoga kwa mwanaume mdogo na mmoja wa wahudumu bora wa umma.

Alielezea jinsi alivyofanya kazi karibu na marehemu mtoto wake wa kiume, Beau, alipokua Mwanasheria Mkuu wa California. “Nilishuhudia walipochukua benki kubwa, wakawainua wafanyakazi, wakawalinda wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji”. “Nilijjivunia sana wakati huo, najivunia sasa kuwa nae kama mwenzangu katika kampeni hii .”

Baadae Kamala naye alitweet “Nina heshima kujiunga nae kama mtu aliyeteuliwa na chama kugombea kiti cha Makamu wa Rais na kufanya yapasayo kumfanya awe Amir jeshi .”

Kampeni ya chama ilitangaza kuwa Biden na Harris watatoa hotuba zao katika Wilmington, Delaware, Jumatano juu ya “jinsi watakavyofanya kazi kwa pamoja kurejesha moyo ya taifa na kupigania familia zinazofanya kazi kuendeleza mbele taifa “.

Biden aliahidi mwezi Machi kwamba atamtaja mwanamke kugombea wadhifa wa Makamu wa rais. Alikabiliwa na miito mingi kumteua mwanamke mweusi katika miezi ya hivi karibuni wakati taifa lilipokua likikumbwa na maandamano ya kijamii juu ya ukatili wa polisi dhidi ya Wamarekani weusi.

Wakati mwingine uteuzi unaotarajiwa ni kwa ajili ya sababu inayotarajiwa. Kamala Harris alikua wa mstari wa mbele katika wagombea wa Makamu wa rais hususan tangu wakati ulipotangazwa uteuzi wa Democratic mwezi Machi ambapo Biden alitangaza kuwa atamteua mwanamke kwa tiketi ya mgombea mwenza.

Ni mdogo kwa umri na mwenye nguvu za kuzungumza katika televisheni, na kama binti wa mhamiaji Mjamaica na Muhindi anawakilisha kuongezeka kwa utoaji wa fursa kwa watu wa jamii mbali mbali katika chama cha Democratic.

Zaidi ya hayo, anafahamika kupitia vyombo vya habari, kwa kampeni zake za kuwania urais mwaka 2019 na kwa muda katikakati ya mwaka jana baadhi ya kura za maoni zilimuweka katika nafasi ya kwanza.

Wengi miongoni mwa mahasimu wake katika kuwania kiti cha Makamu wa rais hawakufikia kiwango cha kuchunguzwa cha aina hiyo, kwahiyo hapakua na ushahidi kwamba wangeweza kuhimili wadhifa huo.

Faida nyingine aliyokuwa nayo ambayo inapuuzwa kumuhusu Harris ni urafiki aliokuwa nao na Marehemu mtoto wa kiume wa Biden, Beau, ulioanzishwa wakati wote walipokua wanasheria wakuu. Biden anathamini sana familia -na uhusiano huo huenda ulimrahisishia kumchagua.

Sasa Harris atakuwa na fursa ya kuanza kampeni tena na kuthibitisha kuwa anastahili uteuzi huu wa kihistoria. Kama atafanikiwa, atakua katika nafasi nzuri ya kutafuta kiti cha urais tena, labda hata mwaka 2024. Leo ameimarisha mizizi yake katika chama cha Demokratic kwa miaka ijayo.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya Biden, kumtangaza seneta Kamala kuwa mgombea mwenza, rais Donald Trump ameukosoa uteuzi huo na kueleza kuwa umekwenda kombo.