VISIWA vyetu vimefungua milango ya biashara na uwekezaji kwa malengo ya kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma na bidhaa kwa wingi, kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa.
Zanzibar kama sehemu ya dunia, haiwezi kukwepa mwenendo wa soko huria la biashara ambalo linaendana na matakwa ya wanaohitaji huduma na bidhaa.
Pamoja na hayo yote, lazima tuwe makini katika kuruhusu bidhaa gani na za aina ipi hasa za mitumba tuziruhusu kuingia nchini mwetu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wetu.
Wapo baadhi wamekuwa na mawazo potofu kwamba eti bidhaa zilizotumiwa nje ya nchi zina ubora kuliko mpya za kupachua madukani. Hatudhani kama hili lina ukweli.
Sio kusudio letu kabisa kuharibu biashara za watu, lakini kiukweli umefika wakati lazima suala la uingizwaji wa biadhaa za mitumba liangaliwe upya kwa sababu Zanzibar inaelekea kuwa jaa la bidhaa zilizokwisha tumiwa nje.
Kwenye soko la Zanzibar, zipo bidhaa nyingi za mitumba zinazoingia ikiwemo gari zilizokwisha choka hasa aina ya Convoy, mitumba ya nguo hadi zile za ndani, mitumba ya vifaa vya umeme kama ma-friji, matairi ya gari nakadhalika.
Ni jambo la kusikitisha sana siku ambayo mzigo wa bidhaa za mitumba unafunguliwa ndipo watu wa mji mzima hjazana kuja kujipatia bidhaa na huduma.
Hatutaki kusema kuwa kila cha mtumba kibovu na hakifai, lakini vyengine jamani imefikia wakati lazima tuseme kweli kuwa havifai kuingizwa nchini mwetu seuze kuruhusiwa wananchi wavitumie.
Kwa mfano, zipo taarifa za kitaalamu kutoka kwa mafundi wa gari zinazoeleza kuwa gari aina ya Convoy za mitumba ambazo hapa Zanzibar zimekuwa mashuhuri kwa kubeba abiria zinazotoka nchini Uingereza, hata spea hazina.
Huko zinakotoka tayari hazitakiwi tena kwa matumizi kiasi cha kutokuwa na spea, lakini huku kwetu tunaruhusu zibebe abiria, jambo ambalo ni kuziweka rehani roho za wananchi wetu.
Gari la Convoy linapoharibika lazima ukimbilie gereji ili ukachongewe kifaa kilichoharibika kwani hakuna duka la vifaa vya gari ambalo unaweza kukipata kifaa unachokihitaji.