NA ABDI SULEIMAN

TAASISI ya Viwango Zanzibar (ZBS) ofisi ya Pemba, imeteketeza kontena lenye pempasi na bidhaa nyengine baada ya kuonekana hazifai kwa matumizi ya binaadamu.

Bidhaa hizo ambazo zilikamatwa Julai 29, 2020, katika bandari ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba zikitokea Unguja, ambazo zinamilikiwa na mfanyabiashara, Abdalla Juma (Miraji) wa Chake Chake.

Zoezi hilo ambalo lilifanyika Pujini wilaya ya Chake Chake, lilishuhudiwa na viongozi kutoka taasisi mbali mbali za serikali na vikosi vya ulinzi na usalama.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Pujini, Kaimu Mkurugenzi dhamana wa taasisi hiyo, Hamad Hassan Chande, alisema wameteketeza bidhaa hizo kwa sababu hazifai kutumiwa na binaadamu.

Aidha alisema lengo la ZBS sio kuwaadhibu wafanyabiashara,  bali ni kutoa funzo kwao na jamii kwamba bidhaa zote zinazohitajika kuingia Zanzibar lazima ziwe na viwango.

Aliwataka wafanyabiashara wanaoangiza biashara hasa kutoka nje, kuhakikisha wanapita katika taasisi hiyo, ili kupata maelezo ya kina na kujiridhisha kabla ya kuagiza mizigo hiyo.