NA HAJI NASSOR

SHIRIKA la Bima la Zanzibar, limekutana na mashesha wa mikoa miwili ya Pemba juu ya umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kujiunga na bima.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Abdulnasir Ahmed Abdulrahman, alipokuwa akijibu hoja za masheha kwenye mkutano wa siku moja uliofanyika kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi.

Alisema, masheha ni kiungo muhimu kati yao na wananchi, hivyo kama wakiitumia vyema nafasi yao, inaweza kusaidia wananchi weng, kukata bima wao au mali zao, ili iwe rahisi wanapokumbwa na majanga kufidiwa.

Alisema serikali ilianzisha shirika hilo kwa nia njema, ili kuhakikisha wananchi wanapokumbwa na majanga kama vile ajali, kuunguliwa moto nyumba zao, kuibiwa, kuzama au kupotea kwa vyombo vyao wafidiwe.

Alifahamisha kuwa, serikali kupitia makusanyo yake imewekeza fedha kwenye shirika hilo, hivyo ni nafasi kwa wananchi kujiunga nalo.

Katika hatua nyingine, alisema ndani ya shirika hilo hakuna ugumu wala kuchelewesha malipo ya bima kwa wanachama wao.

Alisema, kinachojitokeza wapo baadhi ya watu huacha kukata bima za vyombo au mali zao lakini mara tu wanapopata ajali hukimbilia kukata bima.

Hata hivyo, alisema kwa sasa shirika hilo linafanya kazi zake kisayansi zaidi, kwa kuongeza matawi yake katika maeneo kadhaa ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Akiwasilisha mada ya biashara na madai, Mkurugenzi Mratibu kanda ya Tanzania Bara wa shirika hilo, Imam Ali Makame, alisema ili kuwafikia wananchi wengi, wameanzisha utaratibu wa kuweka mawakala.

Alisema, wanazo aina mbili kuu za bima ikiwa ni pamoja na bima kubwa (comprehensive) ambapo ni mpango maalum unaotoa kinga kwa chombo husika na mtu wa upande wa tatu, au mteja anapopatwa na ajali.