NA ABOUD MAHMOUD
UBALOZI wa heshima wa Brazil umesema utahakikisha Zanzibar inapata nafasi kubwa duniani katika mchezo wa soka la ufukweni kama zilivyo nchi nyengine.
Hayo yamesemwa na Balozi wa heshima wa Brazil Zanzibar, Abdusamad Abdulrahim wakati alipofika katika uwanja wa Bububu na kukutana na kamati ya soka la ufukweni ikiongozwa na mshauri mkuu wa mchezo huo Ali Shariff ‘Adolph’.
Abdulsamad alisema kutokana na mchezo huo kuwa maarufu duniani na umefanikiwa kuitangaza vyema Brazil,ni wajibu wao kuhakikisha Zanzibar inapata nafasi kubwa.
Alisema sio watu wengi wenye kufahamu umuhimu wa mchezo huo, ambao husaidia katika kuitangaza nchi vyema kupitia sekta ya michezo na utalii kwa ujumla.
“Mchezo wa soka la ufukweni ni mmoja wa michezo maarufu duniani na kwa upande wa Brazil imeweza kusifika duniani kutokana na soka hilo ,hivyo malengo yetu kwa ofisi yangu ikishirikiana na kamati hii kuhakikisha Zanzibar nayo inapata umaarufu mkubwa na kutambulikana dunia nzima kupitia soka hili,”alisema.