BIRLIN, Ujerumani
MECHI za Ligi Kuu ya Soka ya Ujerumani ‘Bundesliga’ huenda zikabakia bila ya mashabiki hadi mwaka ujao baada ya Kansela, Angela Merkel, kutangaza zuio la mikusanyiko mikubwa litarefushwa hadi Disemba 31.

Merkel alikutana na magavana wake 16 wa majimbo juzi kujadili jinsi ya kusongeza mbele shughuli za kila siku wakati maambukizi ya virusi vya ‘corona’ yakipanda tena Ujerumani.

Michezo haikuwa mada kuu ya mazungumzo hayo, lakini, inahusika na uamuzi wa kurefusha marufuku dhidi ya mikusanyiko ambayo usafi na ufuatiliaji haviwezi kuhakikishwa.

Marufuku hiyo awali ilistahili kumalizika Oktoba 31, lakini, imerefushwa kwa miezi mengine miwili.

Wakuu wa magavana wa majimbo wataunda kikundi cha kuzingatia uwezekano wa watazamaji kuhudhuria hafla na kuripoti matokeo yao ifikapo mwishoni mwa Oktoba.
Wakati huo huo nchini Hispania, inaelezwa nyota wa Barcelona, Lionel Messi, alimwambia kocha wake wa zamani, Pep Guardiola, wiki iliyopita kuwa alinuia kuondoka Barcelona.

Guardiola, ambaye alikuwa bosi wa Messi kwa miaka minne kwenye dimba la Camp Nou, alimwambia mchezaji huyo atazungumza na wamiliki wa ManCity kuhusu uwezekano wa kumsaini.

Tovuti za Goal na Spox ziliripoti jzui kuwa mawasiliano ya simu yalifanyika kati ya Messi na Guardiola, ikionekana ni ishara zaidi kuwa ManCity wapo katika nafasi ya kwanza kumsaini mchezaji huyo anayesakwa mwenye umri wa miaka 33.


Ofisa Mkuu Mtendaji wa ManCity, Ferran Soriano, tayari yuko Catalonia ambako anatarajia kuzungumza na baba wa Messi, Jorge katika wiki ijayo.

Messi alicheza chini ya Guardiola kuanzia 2008 hadi 2012. Wawili hao walishinda pamoja makombe mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya miongoni mwa mataji mengine mengi.

Messi aliwasilisha nakala kwa Barcelona akieleza kuwa anataka kuondoka kwa uhamisho huru, lakini, miamba hiyo hawaamini anaweza kukitumia kipengee cha mkataba wake ambacho kilimruhusu kufanya hivyo kabla ya Juni 10.(AFP).