BERLIN, Ujerumani
MATUMAINI ya klabu za soka zinazoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ juu ya kurejea kwa uchache viwanjani kwa mashabiki wao wakati msimu mpya wa ligi hiyo utakapoanza mnamo Septemba 18 mwaka huu, yameyeyuka.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, klabu 36 katika ligi kubwa mbili za juu nchini Ujerumani zilikubaliana vipengele vinne vya mapendekezo kutoka katika bodi ya ligi (DFL), ambavyo vingeliwezesha kuona mashabiki wakirejea viwanjani licha ya kuwepo na mripuko wa virusi vya ‘corona’.

Klabu zilikubaliana kuuza tiketi za kibinafsi kwa ajili ya kufuatilia watazamaji, na hakuna mashabiki kutoka timu pinzani kwa mwaka 2020, hakuna pombe iliyoruhusiwa hadi mwezi Oktoba na mashabiki wakiwa wameketi tu kwenye viti, na maeneo ya veranda uwanjani yakibakia wazi. Hata hivyo, lazima kwanza upitishwe na serikali ya Ujerumani.

Mwanasiasa Dilek Kalayci, ambaye ni mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa afya wa Ujerumani waliokutana juzi na alimwaga maji baridi kwenye matumaini ya ligi hizo.

“Hatupo tayari kupitisha maamuzi juu ya dhana ya usafi wa DFL, “Kalayci aliliambia gazeti la Berliner Morgenpost kabla ya mkutano. “Kandanda la kulipwa halipo katika orodha ya vipaumbele vya kwanza kwa mawaziri wa afya”.

Klabu za soka zilizoko katika ligi kuu ya soka nchini Ujerumani, zimepoteza mamilioni ya euro yatokanayo na viingilio kwa kila mechi ya nyumbani zilizokuwa zikichezwa bila ya kuwa na mashabiki uwanjani.

Ingawa, idadi ya maambukizi ya virusi vya ‘corona’ inaongezeka kidogo nchini Ujerumani na visa vipya 436 vikiripotiwa katika saa 24 zilizopita na jumla ya vifo karibu 9,000 vikiripotiwa.

Mechi tisa za mzunguko wa mwisho wa ligi ya Bundesliga katika msimu uliopita zote zilichezwa huku milango ya viwanja ikiwa imefungwa kuzuia mashabiki kuingia uwanjani.

Rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani, Frizt Keller, alipendekeza wazo la mashabiki kufanyiwa vipimo katika msimu ujao, lakini, Kalayci akatupilia mbali wazo hilo.
“Wazo la kwamba, miongoni mwa vitu vingine, mashabiki wote viwanjani wanaweza kufanyiwa vipimo liliangaliwa kwa kupingwa na idadi kubwa ya mawaziri”, aliongeza Kalayci.(AFP).