NAIROBI, KENYA

BUNGE  la Seneti ya Kenya linajadiliana kuhusu mvutano unaougusa  Mswada tata wa ugavi wa mapato .

Chama cha Jubilee kiliwaonya vikali Maseneta waasi ambao walipinga pendekezo la Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata wiki iliyopita kuhusu mfumo wa kuzingatia idadi ya watu kwa kaunti.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe aliwaonya Maseneta saba wakiwemo Johnson Sakaja, Kipchumba Murkomen na Anwar Loitiptip ambao wanaendeleza vugu vugu kwa jina la ”One Kenya Movement” wakilenga kuhakikisha kuwa hakuna kaunti inayopoteza mgao wa fedha.

Aidha,Seneti itajadili mapendekezo ya Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja anayeshinikiza mfumo wa sasa  ufanyiwe marekebisho na kutumika kusambaza fedha kwa kaunti kuhakikisha kuwa kila kaunti inapewa mgao unaostahili.

Hata hivyo Maseneta Mutula Kilonzo Jnr na Cleophas Malala miongoni mwa wengine,wanapania kuwasilisha mapendekezo mapya yanayounga mkono yale ya Sakaja. 

Mutula alisema kuwa hatokubali baadhi ya kaunti kunufaika na nyengine kutengwa.

Murathe ambaye awali alifanya kikao na  Kinara wa ODM Raila Odinga,  aliwashauri Maseneta kupitisha mapendekezo ya CRA kuhusu mfumo unaopigiwa upatu wa idadi ya watu kwa kaunti.

Hayo yanajiri huku Magavana wakishindwa kuafikiana na hazina ya Kitaifa na Tume ya Ugavi wa Mapato kuhusu shilingi bilioni 29 za bajeti ya mwaka wa kifedha uliopita.

CRA ilisema iko tayari kuidhinisha asimilia 50 ya fedha hizo kwa kaunti iwapo mzozo wa ugavi wa mapato hautopata suluhu, suala linalopingwa na Magavana wanaosema huduma kwa kaunti zinataendelea kutatizika.