GITEGA,BURUNDI

VYOMBO vya habari nchini Burundi vimeripoti kuwa Serikali ya nchi hiyo inapanga kuziandikia Ujerumani na Ubelgiji, zilipe kiasi cha uro bilioni 36 kama fidia ya utawala wa kikoloni.

Radio ya kimataifa ya Ufaransa ilisema seneti ya nchi hiyo imeunda jopo la wataalamu watakaotathmini uharibifu uliofanywa enzi za ukoloni na kushauri juu ya gharama ya uharibifu huo.

Burundi inapanga pia kuyataka mataifa ya Ulaya kurejesha mabaki ya kihistoria yaliyoibiwa na vifaa vyengine vya kumbukumbu.

Kutoka mwaka 1890, Ujerumani iliitawala Burundi, ambayo ilikuja kuwa sehemu ya Ujerumani ya Afrika Mashariki.

Baada ya vita vya kwanza vya dunia, taifa hilo lilitawaliwa na Ubelgiji hadi ilipojipatia uhuru wake mwaka 1962.

Burundi sasa inaungana na Namibia ambayo imekuwa kwenye mazungumzo na Ujerumani ya kutaka fidia na kuombwa msamaha kwa uhalifu uliofanywa enzi za ukoloni.