NA HAFSA GOLO
WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico amewasihi wanawake wajane kujidhatiti na kupigania haki zao ili kujiendeleza kimaisha.
Aidha aliwataka kutokubali kutumika na ngazi na vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu badala yake waamini serikali kuwa itaendelea kuwapatia fursa za maendeleo ili waondokane na changamoto za kiuchumi.


Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar(ZAWIO) uliofanyika katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo, mjini Unguja.
Alisema ni vyema wakatambua kwamba serikali imeweka mipango na mikakati mizuri ya kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya kujikwamua na umasikini sambamba na kuimarika kimaendeleo.


“Jambo la msingi ni kufuata maelekezo na taratibu zilizopo hasa ikizingatiwa serikali imekuwa mstari wa mbele kusimamia haki na maslahi mapana ya wanawake ikiwemo kuandaa mazingira mazuri ya upatikanaji wa elimu bora,” alisema.
Hivyo,aliwasisitiza umuhimu wa kujielewa na kutambua haki zao pamoja na kujenga utamaduni wa kushirikiana na kuimarisha umoja katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili sambamba na masuala ya maendeleo.


“Fanyeni kazi kwa upendo na amani na wala msikubali vitisho ili mfikie malengo mliojiwekea,” alisisitiza.
Alifahamisha kwamba mpango wa kupatiwa elimu wanaweke ni miongoni mwa mambo muhimu katika mwenendo mzima wa maisha yao ya kila siku hasa ikizingatiwa ni
“Mwanamke ni kiongozi bora na mwenye kuihudumia vyema familia bila ya kujali changamoto zinazomkabili hupambana ili kuhakikisha mahitaji yote muhimu kwa watoto yanapatikana,” alisema


Akizungumzia kuhusu udhalilishaji dhidi ya wanawake alisema,sheria za nchi zikiongozwa na katiba zote mbili zimeeleza wazi kuwa kila mtu yupo huru na hapaswi kunyanyaswa kwa namna yoyote ile.
Aliwaasa wale ambao wamekuwa wakitumia nguvu zao kuwadhalilisha wanawake katika ndoa na nje ya ndoa waache mara moja aidha na wale waliofanyiwa na wanaofanyiwa wasiendelee kunyamaza bali waripoti katika maeneo husika ili sheria ichukue nafasi yake.


Mbali na hilo, alisema amezisikia changamoto zinazoikabili ZAWIO ikiwemo ukosefu wa usafiri, ofisi na vifaa na kueleza kwamba ni suala linalozungumzika na kupatiwa ufumbuzi unaostahiki kwa kuzingatia maslahi mapana ya wanawake wajane na taifa kwa jumla.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya ZAWIO Mgeni Hassan Juma aliiahidi jumuia hiyo kutokana na uwezo wa serikali watarajie mambo yao yatakuwa mazuri na watafikia malengo waliojipangia ya maendeleo.


Akimkaribisha mgeni rasmi, mwenyekiti wa jumuiya hiyo Tabia Makame Mohammed alieleza kuwa lengo la jumuiya hiyo imeanzishwa ili kusaidia kujenga uwezo wa wanawake wajane kujitegemea.
“Wanawake wajane wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya malezi ya watoto, hivyo ZAWIO ina lengo la kuwaunganisha na kutafuta njia za kutatua changamoto zinazowakabili,” alieleza Tabia.


Mkutano huo ulioambatana na uzinduzi wa jumuiya hiyo, mbali ya wanawake wajane wa maeneo mbali mbali ya unguja, pia ulihudhuriwa na Mwalimu wa ujasiriamali na mjumbe wa kamati tendaji ya chama cha wanawake wajane Tanzania bara (TAWIA) Sabrina Tenganamba aliewakilisha chama hicho katika mkutano huo.