NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KIUNGO Mzambia, Clatous Chotta Chama ameshinda tuzo mbili katika sherehe za Tuzo za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilizofanyika usiku wa jana ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Chama amechukua Tuzo ya Mchezaji Bora ambayo imempatia donge nono la Sh. Milioni 10 baada ya kuwashinda mabeki Mganda Nicolas Wadada wa Azam FC na Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union.

Tuzo ya Kiungo Bora Chama amewashinda Lucas Kikoti wa Namungo FC na Mapinduzi Balama wa Yanga SC) na kuzawadiwa Sh. Milioni 3.

Aishi Manula wa Simba SC ameshinda tuzo ya Kipa Bora akwaangusha Mburkinabe Nourdine Balora wa Namungo FC na Daniel Mgore wa Biashara United na kuzawadiwa Sh. Milioni 10.

Nico Wadada wa Azam FC akashinda tuzo ya Beki Bora dhidi ya Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union na David Luhende wa Kagera Sugar na kuzawadiwa Sh. Milioni 3.

Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ikaenda kwa Novatus Dissmas wa Biashara United aliyewashinda Dickson Job wa Mtibwa Sugar na Kelvin Kijiri wa KMC na kuzawadiwa Sh. Milioni 3.

Tuzo ya Bao Bora ikaenda kwa Patson Shikala Mbeya City kwa bao lake alilofunga dhidi ya JKT Tanzania, akwashinda Sadallah Lipangile wa KMC na bao lake alilofunga dhidi ya Mtibwa Sugar na Luis Miquissone wa Simba na bao lake alilofunga dhidi ya Alliance na kuzawadiwa Sh. Milioni 3

Tuzo wa Kocha Bora imechukuliwa na Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck wa Simba SC aliyewashinda Mnyarwanda Hitimana Thiery wa Namungo FC na Mromania Aristica Cioaba wa Azam FC na kuzawadiwa Sh. Milioni 7.

Tuzo ya Mwamuzi Bora imechukuliwa na Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam aliyewashinda Ahmed Arajiga wa Manyara na Abdallah Mwinyimkuu wa Singida na kuzawadiwa Sh. Milioni 6.

Mwamuzi Msaidizi ni Frank Komba wa Dar es Salaam pia aliyewashinda Abdulaziz Ally wa Arusha na Hamdani Said wa Mtwara na kuzawadiwa Sh. Milioni 6.

Seti Bora ya Waamuzi; Athumani Lazi wa Morogoro, Abdallah Mwinyimkuu wa Dar es Salaam, Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono wa Tanga kila mmoja amepata Sh. Milioni 2.

Kagera Sugar ya Bukoba ikashinda Tuzo ya Timu yenye Nidhamu dhidi ya Coastal Union ya Tanga na Mwadui FC ya Shinyanga na kuzawadiwa Sh. Milioni 15.

Aishi Manula, Nico Wadada, David Luhende, Bakari Mwamnyeto, Pascal Wawa wa Simba, Zawadi Mauya wa Kagera Sugar, Lucas Kikoti, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco wa Simba SC na Luis Miquissone wakateuliwa kuunda kikosi Bora cha Msimu cha Ligi Kuu na kupewa Tuzo.

Gwiji Sunday Ramadhan Manara akapewa Tuzo ya Heshima kutokana na mchango wake mkubwa katika soka ya nchi hii, akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka ya kulipwa Ulaya, baada ya kusajiliwa na Heracles ya Uholanzi mwaka 1978.

Manara aliyekwenda Ulaya akitokea Pan Africans alikocheza kwa muda mfupi akitokea Yanga SC, iliyomuibua kuanzia timu ya vijana amezawadiwa Sh. Milioni 3 kwa ushindi wa tuzo hiyo ya Heshima aliyokabidhiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mfungaji Bora Meddie Kagere wa Simba SC aliyemaliza na mabao 22 mbele ya Yussuf Mhilu wa Kagera Sugar, Peter Mapunda wa Mbeya City wote mabao 13, Waziri Junior wa Mbao FC mabao 12 sawa na Obrey Chirwa wa Azam FC na Reliant Lusajo wa Namungo FC ameondoka na Sh Milioni 10.

Bingwa wa Ligi Kuu, Simba SC amezawadiwa Sh. Milioni 100, washindi wa pili, Yanga SC Sh. Milioni 45, wa tatu Azam FC, Milioni 30 na wa nne, Namungo FC Milioni 10.