SHIRIKA la anga za juu nchini Marekani (NASA), limezindua chombo kipya cha anga za juu kilichopewa jina la Perseverence ambapo kimeanza safari kuelekea sayari ya Mars kufanya utafiti.
Kwa mujibu wa taarifa chombo hicho kipya kurushwa kwenda kwenye sayari hiyo ni cha tano kurushwa na shirika la NASA na ndicho kikubwa na kizito zaidi ikilinganishwa na vyombo vilivyorushwa awali.
Mnamo mwanzo wa Julai mwaka huu, wahandisi wa NASA walikiweka chombo Perseverence cha kuelekea Mars kwenye roketi ya Atlas V. Roketi hiyo ilirushwa Julai 30 katika eneo la Cape Canaveral liliopo mjini, Florida. Chombo hicho kinatarajiwa kuwasili katika sayari ya Mars mnamo Februari mwaka 2021.
Chombo ambapo awali kilioneshwa kwa umma mwaka 2019, kitasaidia chombo kilichotangulia kwenye safari hiyo kilichorushwa na NASA kilichopewa jina Curiosity ambacho nacho kimekwenda katika katika sayari Mars.
Curiosity ndicho kilikuwa chombo cha kisasa zaidi hadi Perseverence kilipotengenezwa. Perseverence kina uzito wa tani moja zaidi ya Curiosity. Kina urefu wa mita tatu, ambayo ni sentimita 10 zaidi ya urefu wa Curiosity.
Chombo Perseverence kinaweza kuwekewa vifaa zaidi vya utafiti kuliko Curiosity. mikono yake, kamera na vifaa vyengine vina nguvu zaidi. Chombo hicho kinaweza kukusanya sampuli pale kitakapofika katika sayari ya Mars.
Kimewekewa kamera 23 na vifaa vyengine, lengo ni kubaini uwezekano kama kwenye miamba ya sayari hiyo kuna hewa safi yaani oksigeni.
Chombo Perseverence kina helikopta aina ya drone. Hilo halijawahi kufanyika kwa vyombo vya anga za juu vinapoelekea kutafiti sayari nyingine, matumizi ya helikopta ni jambo jipya kabisa.
Itakuwa mara ya kwanza watafiti wataijaribu na kuitumia kukusanya data katika anga hewa ambayo ni tofauti na ya dunia na pia katika mvuto wa sayari yaani ‘gravity’ ambao ni theluthi moja ya wa dunia.
Chombo Curiosity ndicho kilikuwa kikubwa na cha kisasa zadi kupelekwa Mars, ambapo kiliwasili Agosti 16, 2012 na tayari kimefanya safari ya kilomita 21. Si chombo tu kinachosafiri. Jina lake rasmi ni Maabara ya Kisayansi ya Mars na kwa hakika ni maabara kamili inayosafiri.
Kwa mfano, kina vifaa vya kupima kemikali zitakazogunduliwa Mars, kina kituo kizima cha utabiri wa hali ya hewa kinachoweza kupima viwango vya joto, presha angani, mionzi, unyevu, kasi ya upepo, lakini ya muhimu zaidi ni kwamba kina maabara ya kemia kinachoweza kufanya tathmini ya sampuli za vitu vilivyomo humo kando na kutafuta alama ya ikiwa kuna viumbe.
Kinadharia, chombo Curiosity kimeonyesha kuna uwezekano wa kuwa na uhai katika sayari Mars. Lakini bado hakijabaini kiumbe chochote hai kilihcopo katika sayari hiyo. Chombo hicho kina kifaa madhubuti cha kuchimba.
Michanga ya Mars hushughulikiwa na vyombo vingi. Kwanza huchujwa, kuchungwa na kugawanywa katika mafungu tofauti kulingana na saizi zao. Kisha unafanyiwa vipimo tofauti kutumia mashine mbalimbali kwenye maabara.
Vyombo vilivyokitangulia Curiosity kupelekwa Mars, vilikuwa vidogo. Mnamo Julai 4, 1997, chombo kidogo kwa jina Sojouner, kiliweka alama za magurudumu yake kwenye sayari Mars.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza roboti linalosafiri kuachwa kutegema vifaa vilivyowekewa, ikiwa ni pamoja na chombo cha X-ray pamoja na kamera kufanya vipimo na tathmini.
Ulinganishaji wa ukubwa hadi sasa kuna vizazi vitatu vya vyombo vya anga za juu kuitafiti sayari ya Mars. Sojourner ilikuwa na uzito wa kilo 10.6. Ukubwa wake ulikaribia wa kijigari kidogo.
Kilikwenda kwa kasi ya sentimita moja kwa sekunde. Chombo kwa jina Opportunity kilikuwa na uzito wa kilo 185. Nacho Curiosity kilikuwa na uzito wa kilo 900, vyombo hivyo vikubwa vinasafiri kwa kasi ya sentimita 4 au tano kila sekunde.
Katika kipindi chake, chombo Sojourner kilisafiri jumla ya mita 100 na kuwasilisha data pamoja na picha hadi Septemba 27, 1997. Hata hivyo chombo hicho kilikata mawasiliano ya redio.

Wataalamu wanaeleza kuwa kuna sababu nyingi zilizosababisha chombo hicho kukata mawasiliano ikiwemo kuharibika kwa betri yake na kushindwa kustahimili baridi nyakati za usiku iliyopo katika sayasi hiyo.
Bila ya data zilizokusanywa na Sojourner, huenda kusingekuwa na fikra ya kuunda vyombo vipya. Mwaka 2004, NASA ilipeleka maroboti mawili Spirit na Opportunity katika sayari Mars.
Spirit ilidumu kwa miaka sita na kusafiri jumla ya kilomita 7.7. Roboti hilo lilipanda milima na lilikusanya sampuli mbalimbali, lakini roboti Opportunity lilipoteza mawasiliano mnamo Februari 13 mwaka 2019.
Mnamo mwaka 2005, roboti Opportunity lilisafiri umbali wa kilomita 42, na hadi leo linaendelea kusafiri kilomita nyingi kuliko chombo Curiosity. Linaweza kutumia mkono wake kuchunguza ardhi.
Roboti hilo lina vifaa vitatu tofauti vya vipimo pamoja na kamera ya 3D. Mara ya mwisho ilikuwa ikifanya utafiti katika bonde la Perseverance kabla ya kuelemewa na kimbunga kutokana na mchanga.
Picha iliyopigwa na kamera ya roboti Curiosity. Chombo cha kisasa zaidi kinaweza kudumu katika sayari Mars kwa muda mrefu zaidi, ikiwezekana miaka isiyopungua mitano.
Muonekano wa ardhi ya Mars unaonekana kuwa wa kawaida. Je unafikiri binaadamu anaweza kwenda katika sayari hiyo ya kuvutia au tuache maroboti yaendelee kwenda huko?