NA MWAJUMA JUMA

TIMU za soka za Chumbuni na Jamaika zimefanikiwa kutinga hatua ya sita bora ya ligi daraja la tatu inayoendelea visiwani hapa.

Timu hizo ambazo zilicheza juzi katika viwanja viwili tofauti kila mmoja iliibuka na ushindi kwenye michezo yao ambayo ilichezwa majira ya saa 8:00 mchana.

Chumbuni ilishuka katika uwanja wa KMKM Maisara na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 , ambayo yalifungwa na Ramadhan Shindano dakika ya 23 na Ame Abdalla dakika ya 89, wakati bao la Mpendae likiwekwa kimiyani na Juma Shirazi Hassan kwa mkwaju wa penalti katika dakika

ya 50.

Kwa upande wa timu ya Jamaica wao walishuka katika dimba la Mao Zedong B kucheza na Sap Soap na kufanikiwa kutoka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Ali Khamis dakika ya 47.

Tayari timu nne zimeshaingia hatua hiyo zikiwemo na Spriti na

Muembemakumbi na sasa zinasubiriwa timu mbili ambazo zitaungana na nne hizo kucheza sita bora.