NA ABOUD MAHMOUD
TIMU ya soka ya Chuoni FC inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar imetangaza kujitoa kushiriki mashindano ya kombe la FA, ambapo mechi yao ilitarajiwa kuchezwa Agosti 11 dhidi ya Dulla Boys.
Kwa mujibu wa barua iliyotiwa saini na Katibu wa klabu hiyo Mattar Salum Mohammed inaeleza kwamba kufuati kikao cha kamati tendaji ya klabu hiyo, kilichokaa Agosti 2 kwa kauli moja kimepitisha azimio hilo la kujitoa kushiriki mashindano hayo yanayoendelea katika hatua ya robo fainali.
Katika barua hiyo ambayo imetumwa kwa kwa Kaimu Katibu Mkuu wa ZFF, imesema lengo la mashindano hayo ni kumpata mshiriki wa mashindano ya Shirikisho,halitofanikiwa kwa vile mwisho wa kutuma majina ya washiriki wa mashindano ilikuwa Julai 31 mwaka huu.
Alisema kutokana na hayo itakuwa ni upotevu wa rasilimali na hakuna kinachofuatwa kwa kutokua na kalenda ya msimu na kuifuata, hivyo kupelekea kutojua namna ya kujipanga kuendesha timu.
Barua hiyo ilifafanua kuwa kutokana na hali hiyo timu hiyo haina uwezo wa kuendesha timu kwa mwezi mmoja kwani ratiba waliyoipokea inafikia mwisho wa mwezi huu.
Ilifafanua kuwa Chuoni FC haina uwezo wa kuendesha timu kwa mwezi mmoja zaidi ya kuhudumia kama ratiba walioipokea, inafika hadi mwisho wa mwezi wa Agosti 2020.
Kwa mujibu wa barua hiyo ukaguzi wa klabu hadi hivi sasa haujafanyika wa kupatiwa leseni za msimu ujao 2020/2021, hivyo kutoweza kufanikisha suala hilo, na kwa kawaida klabu iliyokuwa haikuwahi kukaguliwa hata mara moja.
Kutokana na hilo timu hiyo itakosa vigezo pia muda wa ukaguzi kufanyika ili kushiriki mashindano ya CAF.
Hivyo kutokana na hayo Chuoni FC imejitoa rasmi kwenye mashindano hayo ili kujipanga na mambo ya klabu kwa msimu ujao.