BOGOTA,COLOMBIA

COLOMBIA  imesema bado ina matumaini kuwa kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji wenye silaha Salvatore Mancuso atarejeshwa nchini humo licha ya uamuzi wa Marekani wa kumsafirisha kwenda Italia.

Kamishna wa Tume ya amani nchini Colombia Miguel Ceballos alisema nchi hiyo bado haijafahamishwa rasmi kuhusu Mancuso kupelekwa Italia lakini haijakata tamaa kwamba mtuhuhuwa huyo wa uhalifu atarejeshwa Colombia kujibu tuhuma zinazomkabili.

Wizara ya sheria ya Marekani ilisema Mancuso atapelekwa Italia licha ya maombi matatu ya Colombia na polisi ya kimataifa Interpol ya kutaka akabidhiwe kwa Colombia kujibu mashitaka ya mauaji ya mamia ya watu. Mancuso, mmoja wa viongozi wa kundi hatari la wapiganaji wa kijeshi la AUC nchini Colombia alipelekwa Marekani mwaka 2008 kutumikia kifungo gerezani kwa usafirishaji wa dawa za kulevya.