NA NIZAR VISRAM, OTTAWA
MNAMO mwezi Aprili mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alizungumzia suala la deni la kimataifa jinsi lilivyokuwa mzigo mzito kwa nchi za Kiafrika hasa wakati huu ambapo bara zima linakabiliwa na janga la virusi vya corona.
Akitoa mfano wa Tanzania alisema nchi hii inalipa takriban shilingi bilioni 700 kila mwaka kwa wakopeshaji wetu. Katika fedha za kigeni hii ni zaidi ya dola milioni 300. Hizi ni fedha zinazotoka nje ili kulipa madeni na riba, yaani kuhudumia madeni.
Dk. Magufuli alisema Benki ya Dunia (WB) peke yake inachukua kati ya shilingi bilioni 200 na 330 kila mwaka, sawa na dola milioni 129.
Raia Magufuli akawataka wadeni wetu, ikiwemo Benki ya Dunia (WB), wafute madeni yao wanazozidai nchi za kiafrika kama njia ya kuzisaidia kupambana na janga la virusi vya corona. Fedha hizi zinazotoka nje kila mwaka zingezaidia katika kujikinga na corona.
Dk. Magufuli alisema ni vizuri nchi za Kiafrika zingeungana na kudai madeni yao yafutwe badala ya kuomba wakopeshwe fedha zaidi, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajiongezea mzigo wa madeni na matokeo yake watakuwa wanalipa fedha zaidi kama riba.
Magufuli alizungumza haya wakati mawaziri wa fedha kutoka nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani (G20) walipokutana na kamati ya maendeleo ya Benki ya Dunia.
Mawaziri hao wakapitisha maamuzi kuwa benki hiyo (WB) pamoja na mfuko wa fedha duniani (IMF) waruhusu nchi 73 masikini wasitishe ulipaji wa riba kwa madeni yao wakati huu nchi hizo zikipambana na janga la virusi vya corona.
Huo ni “msaada” waliouita ‘Debt Service Suspension Initiative’ (DSSI). Usitishaji huu ni kuanzia mwezi Mei hadi mwishoni mwa 2020. Usitishaji huu ni kwa madeni yanayodaiwa na WB na IMF. Madeni kutoka mabenki binafsi na nchi wakopeshaji hayakuhusishwa.
Uchumi wa nchi za Kiafrika kwa ujumla zinaathirika sana kutokana na mambo kadha. Nchi zinazozalisha na kusafirisha mafuta zimeathirika kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta kwenye soko la ulimwenguni.
Pamoja na hayo sasa nchi hizo zinakabiliwa na janga la corona ambalo limeathiri sana uzalashaji na uchumi. Inakisiwa kuwa mnamo mwaka 2020 serikali za Afrika zitapoteza mapato ya dola bilioni 45 kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta sambamba na mripuko wa virusi vya corona.

Zaidi ya hayo nchi zetu zinaumia pia kutokana na kuanguka kwa thamani ya sarafu zetu. Hii inapaisha ulipaji wetu wa madeni na riba. Ulipaji huu unaongezeka kwa dola takriban bilioni 40 kila mwaka.
Kutokana na haya uchumi wa Afrika uliokuwa ukiongezeka sasa unapungua. Tayari watu takriban 20,000 wamepoteza maisha yao kutokana na corona barani Afrika. Kati yao zaidi ya 8,000 ni kutoka Afrika Kusini.
Wachambuzi wanasema janga hili limewafukarisha Waafrika milioni 12 na idadi hii inazidi kuongezeka. Nchini Kenya na Senegal, kwa mfano, asilimia 80 ya wafanyakazi wamepoteza ajira zao. Afrika Kusini zaidi ya watu milioni 8 hawana kazi.
Tatizo kubwa ni kuwa nchi nyingi barani Afrika hivi sasa zimejikita zaidi katika kupambana kudhibiti ugonjwa wa corona. Matokeo yake matumizi mengi yanaelekea kwenye corona badala ya magonjwa mengine kama kifua kikuu, ukimwi na malaria.
Matokeo yake ni kuwa vifo kutokana na magonjwa haya matatu vitaongezeka maradufu kwa sababu ya kupuuzwa huku mataifa ya Afrika yakiutumia macho zaidi ugonjwa wa corona.
Kuhusu madeni ya Afrika ni vizuri ikaeleweka kuwa fedha nyingi zaidi zinatoka nje kuliko fedha zinazoingia kama mikopo.
Katika muda wa miongo minne iliyopita Afrika hasa eneo lililo kusini mwa jangwa la sahara, imepoteza zaidi ya dola bilioni 700 zilizotoroshwa nje kwa kutumia njia mbali mbali.
Ni vigumu kupata tarakimu sahihi juu ya kima halisi cha fedha zinazotoroshwa nje ya Afrika kwani fedha zinatoroshwa nje kisirisiri, wakati mikopo wanayotupa inatangazwa waziwazi.
Hata hivyo, inakisiwa kuwa nusu ya mikopo tunayopokea kutoka nje inarudi huko huko ilikotoka. Yaani mtu anadai anakukopesha shilingi 10,000, lakini anakupa nusu yake na nusu anabaki nayo. Mwishowe were unaishia kudaiwa 10,000. Halafu tunatakiwa tuwashukuru kwa mikopo yao.
Tuwashukuru kwa mikopo wanayotuapatia ama tuwalaani kwa unyonyaji wanaotufanyia unaozifanya nchi zetu ziendelee kuwa masikini.
Pia sehemu kubwa ya misaada huporwa na baadhi ya watawala wa Afrika na kufichwa katika mabenki ya Ulaya (off-shore banks). Mfano mmoja ni ile mikopo aliyopewa dikteta Mobutu wa Zaire.
Mikopo aliitorosha na kuificha huko Ulaya, pamoja na uporaji wa madini na rushwa.Inakisiwa alipora kati ya dola bilioni 4 na 15. Mobutu akapinduliwa na Rais Kabila akarithi madaraka pamoja na mzigo wa madeni ya Mobutu.
Hali kadhalika huko Afrika Kusini utawala wa makaburu ulikopa fedha kutoka nchi za magharibi ili kusaidia serikali yao kupigana na vyama vya ukombozi na kuwagandamiza wananchi. Mandela aliposhika madaraka alitakiwa alipe madeni ya makaburu.
Hali ya sasa ya madeni barani Afrika inazidi kuwa mbaya kutokana na kuibuka kwa janga la corona. Uchumi utazidi kuathirika na wakati huohuo tutakabiliwa na ulipaji wa madeni na riba. Inawezekana tukashindwa kuendelea kuhudumia madeni au huenda vita dhidi ya corona vikashindikana kutokana na kuelemewa na madeni.
Shirika la kimataifa la Oxfam lilizionya nchi tajiri kuhusu hali hii wakati mawaziri wa fedha wa G20 walipokutana baina ya Julai 18 na 19 mwaka huu. Shirika hili liliwaambia mawaziri hao kuwa uamuzi wao wa kusitisha ulipaji wa madeni waliofikia mnamo mwezi Aprili mwaka huu hautafika mbali.
Kwanza usitishaji maana yake fedha usipozilipa sasa hivi utazilipa baadae. Ni kuahirisha ulipaji. Pamoja na hoja hizi, kati ya nchi 73 za Kiafrika zenye sifa za kuomba uahirishaji chini ya mpango wa DSSI ni nchi kama 41 tu zimewasilisha maombi.
Maana yake hawa wako tayari kuahirisha ulipaji wa dola bilioni 9 hadi mwishoni mwa 2020. Miongoni mwa nchi hizo ni Nigeria, Angola, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Comoros, Jamhuri ya Congo, Cote d’Ivoire, Ethiopia, Mali, Mauritania, Niger na Togo.
Hata hivyo, kuna madeni ambayo wataendelea kuyahudumia licha ya DSSI. Mashirika ya Oxfam, Christian Aid na Global Justice Now yameripoti kuwa nchi hizi 73 bado zitalazimika kulipa dola bilioni 33.7 hadi mwisho wa 2020. Kati yake dola bilioni 11.6 zitalipwa kwa wakopeshaji binafsi, yaani mabenki na wawekezaji binafsi. Dola bilioni 13.8 zitalipwa kwa mashirika ya kimataifa kama WB.
Ndipo mashirika hayo yanashauri kuwa mpango wa DSSI uwe kwa madeni yote bila ya kubagua, hadi mwaka 2022. Yanasema kuwa kusitisha ulipaji kwa miezi minane hakutazisaidia nchi change kupambana na Korona. Nchi hizo zitaendelea kuhudumia madeni ya mabenki binafsi bila ya kusita.
Suali la msingi ni iwapo wakopeshaji wa kimataifa watakubaliana na wazo la kufuta madeni yao. Mpaka sasa wachache wao wamekubali kuahirisha tu ulipaji wa riba, lakini siyo kufuta madeni ambayo yamegeuka mzigo mkubwa.

Nchi changa (au nchi za kusini) kwa ujumla zinadaiwa zaidi ya dola trilioni 11. Katika mwaka huu wa 2020 nchi hizi zinapaswa kulipa dola trilioni 3.9. Kulipa fedha zote hizi maana yake ni kushindwa kupambana na corona.
Wakati huohuo nchi hizi zitapaswa kuagiza vyakula kutoka nje baada ya kuwafungia ndani raia wake. Ulipaji wa madeni na riba umekuwa mzigo mkubwa katika nchi za Kiafrika. Mzigo huu umekuwa ukiongezeka.
Mwaka 2015 bara hili lilikuwa linatumia asilimia 5.9 ya mapato ya serikali ili kuhudumia madeni . Mwaka 2017 imefikia asilimia 11.8. Yaani katika miaka miwili tu malipo haya yameongezeka maradufu.
China peke yake inaidai Afrika dola takriban bilioni 4.5. Hii ni asilimia 20 ya madeni yake ya kigeni. Tukiachia China, dola bilioni 13.2 (asilimia 32) tunadaiwa na wakopeshaji binafsi pamoja na hatifungani. Dola bilioni 14.4 (asilimia 35) tunadaiwa na Benki ya Dunia na mashirika mengine ya kimataifa.
Leo hii barani Afrika uhudumiaji wa madeni unameza kiwango kikubwa cha bajeti ya serikali. Mwaka huu wa 2020 bara letu litalipa dola bilioni 3 kama riba kwa wakopeshaji binafsi.
Kiwango hiki kinazidi kuongezeka. Kwa vile wakopeshaji binafsi wanatutoza riba kubwa zaidi, ndipo asilimia 55 ya riba yote tunayolipa inakwenda kwa wakopeshaji hawa.
Nchi nyingi za Kiafrika zinalipa riba ya asilimia 5 hadi 16 kwa ukopaji kupitia hati fungani (bond) ya miaka 10. Hii ni riba kubwa sana ikizingatiwa kuwa watu binafsi wanaoweka akiba zao katika benki za huko Ulaya hawapewi hata riba ya asilimia moja.
Halafu kuna mikopo inayoingia katika mifuko ya wajanja wachache. Ripoti moja ya WB iliyovujishwa inaonesha jinsi asilimia tano ya mikopo na misaada yote ya benki hiyo kwa nchi “masikini” inaporwa na kufichwa katika akaunti za siri huko ughaibuni (tax haven). Ripoti hiyo inasema wizi huu ulizidi katika misaada iliyotolewa kwa nchi 22 kati ya 1990 na 2010.
nizar1941@gmail.com ,+1 613 6992933