LONDON,UINGEREZA
HUDUMA za kupambana na ukatili na ulinzi kwa watoto zimeathirika vibaya wakati huu wa janga la corona au COVID-19 na kuwaacha watoto katika hatari kubwa ya machafuko, unyanyasaji na ukatili kwa mujibu wa utafiti wa kimataifa uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
UNICEF ilisema matokeo ya utafiti huo yaliyotokana na maoni yaliyokusanywa kutoka nchi 104 kati ya nchi 136 kuhusu athari ya kiuchumi na kijamii za COVID-19 yalionyesha kwamba kumekuwa na athari za uingiliaji wa huduma muhimu zinazohusu kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
Utafiti huo unasema takriban theluthi mbili ya nchi ziliripoti kwamba kila huduma iliathirika vibaya ikiwemo Afrika Kusini, Malaysia, Nigeria na Pakistan na nchi za Kusini mwa Asia, Ulaya Mashariki na Asia ya Kati ndizo zilizoripoti kiwango kikubwa cha kuathirika kwa huduma hizo.
Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrieta Fore alisema sasa ndio imeanza kubainika kwa kina athari zinazowasibu watoto kwa kushuhudia ongezeko la machafuko wakati wa hatua za kubakia majumbani kukabiliana na COVID-19.
Kuendelea kufungwa kwa skuli na vikwazo vya kutembea viliwafanya baadhi ya watoto kukwama majumbani na kudhalilishwa.
Athari za huduma za ulinzi kwa wafanyakazi wa huduma za jamii inaonesha kwamba watoto hawana pahala pa kupata msaada.
Ili kukabiliana na hali hiyo UNICEF inazisaidia Serikali,mashirika wadau kuhakikisha zinachukua hatua madhubuti za ulinzi na huduma kwa watoto walioathirika na ukatili wakati wa COVID-19 katika nchi mbalimbali.