NA ASIA MWALIM

UONGOZI wa Hospitali kuu ya Mnazi mmoja umesema umefanya juhudi za kutafuta mafundi wa kutengeneza kifaa cha kufanyia vipimo (CT SCAN) kilichoharibika ili kuendelea na vipimo vyake kama awali.

Msemaji mkuu wa hospitali hiyo, Hassan Makame Mcha, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili huko ofisini kwake Mnazi mmoja, Mjini Unguja.

Alisema kuwa kutokana na kifaa hicho kuwa na tatizo kwa muda wa zaidi ya kipindi cha wiki mbili na kusababisha wananchi kukosa huduma hiyo, ililazimika kutafuta suluhisho la tatizo hilo, linalo ikumba hospitali hiyo.

Alisema tayari wamekamilisha taratibu za kutafuta mafundi na , wamefanya uchunguzi wa kifaa hicho Agost 11, kwani CT SAN kiligunduliwa na tatizo ambalo linatokanana na kifaa cha kuchuja umeme (UPS) kuna wakati huzidiwa nguvu ya umeme na kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Alisema kifaa hicho kina uwezo wa kulinda mashine hiyo sambamba na kujilinda wenyewe pale kinapokuwa kizima, na kinapokuwa na tatizo hakiwezi kuilinda mashine, hali ambayo inapelekea mashine hiyo kuzima na kushindwa kufanya kazi yake. 

“Kutokana na tatizo la UPS ipo haja ya kupata kifaa chengine chenye nguvu zaidi kuliko hicho kilichoharibika”

Aidha amewataka mafundi na Kampuni zinazofunga mashine ambazo zipo chini ya mikataba kufika kwa wakati pale wanapopewa taarifa ya kuharibika vifaa vya hospitali kwani wananchi hupata wakati mgumu.