NA ZAINAB ATUPAE

LIGI soka daraja la pili Wilaya ya Magharibi ’B’ msimu huu imefikia tamati kwa kupigwa michezo mbali mbali  katika viwanja tofauti.

Mchezo uliotimua vumbi uwanja wa Chukwani majira ya saa 8:00 mchana timu ya Villa imetoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kisakasaka.

Mchezo mwengine uliotarajiwa kupigwa majira ya saa 10:00 jioni uwanja huo huo kati ya timu Pangani na Bweni Star, mchezo huo haukufanyika baada ya timu ya Pangani kushindwa kufika uwanjani .

Katika uwanja wa Kiembe Samaki majira ya saa 8:00 mchana timu Hebroni ilitoa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Sanifu,huku mchezo uliotarajiwa kutimua vumbi saa 10:00 jioni, timu ya Kidatu Ranger ilijichukulia pointi baada ya Ndaambani kushindwa kufika uwanjani.

Katika uwanja wa Dimani majira ya saa 8:00 mchana timu ya Eleven Star iliondoka na ushindia mabao 2-1 dhidi ya KU,huku mchezo uliopigwa majira ya saa 10:00 jioni timu ya Azimio ilipata ushindi wa bure baada ya Beach Boys kushindwa kufika uwanjani.

Kwa matokeo hayo timu ya Villa imefanikiwa kuwa bingwa wa ligi hiyo katika msimu wa mwaka 2019-2020 akiwa na pointi 38 na mshindi wa pili ni Eleven Star yenye pointi 33.

Timu ambazo zimeshuka daraja msimu huu ni pamoja na Chem Chem na Sanifuu Harambe.