NA MWANAJUMA MMANGA

WADAU mbalimbali wa maendeleo  wametakiwa kushirikiana na ofisi ya Mamalaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’  pindi wanapotaka kupeleka huduma ya maji kwa wananchi, ili waweze kupata huduma hiyo kwa uhakika.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab, aliyasema hayo  mara baada ya kumaliza ziara hiyo katika baadhi ya vituo vya maji vya Wilaya hiyo, ambapo alisema amebaini  kuwepo kwa matatizo katika baadi ya vituo vya maji kutokana na kukosekana kwa ushirikiano baina ya wadau  na mamlaka hiyo.

Alisema huduma ya maji ni huduma muhimu, hivyo ni wajibu wa kila mdau kushirikiana na Mamlaka hiyo, ili kuweza kuifikisha huduma hiyo kwa kuzingatia vipimo  sahihi pamoja na kuifanya huduma hiyo kudumu kwa muda mrefu.

Alifahamisha kuwa kiujumla hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya hiyo  inaridhisha  licha ya baadhi ya maeneo kukosa  visima vya maji vya mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA), lakini wapo  baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwasaidia  wenzao.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewaahidi wananchi ndani ya wilaya hiyo kuwa ofisi yake itashirikiana na Halmashauri pamoja na   Mamlaka ya maji wilaya kwa kuhakikisha wanayatafutia ufumbuzi baadhi ya matatizo ili huduma hiyo iweze kupatikana bila usumbufu.

Nae Msaidizi Mkurugenzi huduma za jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya hiyo Fakih Juma Khamisi, amewataka wananchi kulinda miundombinu ya maji ambayo imetekelezwa na Halmashauri kupitia mabaraza ya mashauriano ya wadi, ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Ofisa wa Mamlaka ya Maji Zanzibar  wa Wilaya hiyo, Amour Muhammed Silima, amesema baadhi ya maeneo yamekuwa yakikosa huduma ya maji kutokana na miundombinu kuwa ya muda mrefu hivyo amewataka wananchi kuwa wastaamilivu, kwani serikali ipo katika mpango wa kuifanyia marekebisho miundo mbinu hiyo, ili huduma iwe ya uhakika.

Vituo vya maji vilivyotembelewa ni pamoja na kituo cha maji Kipandoni, Kilombero, Kisongoni, Mahonda, Fujoni  pamoja  na. Visima viwili vilivyojengwa na  Halmashauri  ambavyo ni Mgambo pamoja na  Mbaleni,