NA MWANAJUMA MMANGA
KAMPUNI inayoshughulikia ujenzi wa Bandari ya mafuta na gesi katika Shehiya ya Kidanzini kijiji cha Dundua Jimbo la Bumbwini imetakiwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakaazi wa kijiji hicho, ili waweze kunufaika na ujenzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab, aliyasema hayo wakati akizungumza na watendaji wa kampuni hiyo wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo la mradi wa gesi na mafuta ambao umeanza kusafisha eneo kwa ajili ya kujenga matangi na vifaa vyengine.
Alisema kuna baadhi ya kazi hazihitaji utaalamu hivyo ni vyema wakapewa wananchi wa kijiji hicho kwani Serikali imekuwa ikitumia fursa za uekezaji kwa kuhakikisha wanaoishi karibu na maeneo yanayotumika kwa uekezaji wananufaika kwa kiasi kikubwa.
Hivyo Rajab, amewataka wananchi ambao tayari wameshalipwa fidia za mazao yao kuacha kutumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo, ili serikali iweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Nae Injinia wa ujenzi huo, Mohamed Ayoub, amesema tangu kuanza kwa shughuli za ujenzi hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi hali ambayo inawapa uhakika wa kumaliza ujenzi huo kwa wakati.
Alisema katika eneo hilo kutakuwa na matangi mawili yenye ujazo wa lita Milioni nane na matangi mawili yatakuwa na ujazo wa lita Milioni minne ambapo ujenzi huo utatumia muda wa miezi kumi na nne hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake Sheha wa shehiya ya Kidanzini Mussa Ali Mussa, amesema licha ya serikali kulipa fidia kwa wakulima hao lakini tayari ameiomba kampuni hiyo kuwalipa kifuta jasho wananchi ambao waliendelea kulima baada ya kulipwa fidia.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imelitenga eneo la ukanda wa Bumbwimi kuwa eneo la uekezaji wa gesi na mafuta na kwa sasa tayari imeshaanza shughuli za ujenzi kwa ajili ya uekezaji ambapo Ujenzi wa matangi manne unategemewa kutumia eneo la kilomita 6.5 .