NA    ARAFA MOHAMED

MKUU wa Wilaya ya Mjini, Marina Joil Thomas, aliwataka Masheha wa Wilaya hiyo kuunda kamati  maalum itakayoweza  kusimamia majengo ya nyumba  za maendeleo ili  kuyaenzi Mapinduzi  yalio asisiwa na hayati Mzee Abeid Amani Karume.

Aliyasema hayo alipokuwa katika mafunzo maalum kwa Masheha hao, juu ya usimamizi wa nyumba za maendeleo   yalio andaliwa na Bodi ya”KONDOMINO”Zanzibar, katika ukumbi wa elimu Mbalada Raha leo Mjini  Zanzibar.

Alisema, ni vyema kwa masheha hao kuhakikisha wanasimamia   suala la usafi wa mazingira   na kudhibiti uharibifu wa nyumba hizo, unaofanywa na Wananchi wanaoishi katika nyumba hizo, ili kuweza kufikia dhamira iliokusudiwa  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Mrajisi wa   Kondomino Zanzibar, Nadra Makame Othman, alisema lengo la kutoa mafunzo hayo kwa Masheha  ni kutaka kufikisha elimu  kwa Wananchi wao kwa urahisi,  ili kuweka Mji katika haiba nzuri  na yakuvutia.

Sambamba na hayo aliwataka   Masheha hao kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu kwa Wananchi wanaishi   katika majumba hayo ya Maendeleo, ili kuondokana na hali ya uharibifu wa nyumba hizo. Nao baadhi ya Masheha wa Wilaya hiyo, wameishukuru bodi hiyo kwa kuwapa elimu juu ya suala zima  la usimamizi wa nyumba za maendeleo na kusema kuwa ,itawasaidia kujua dhamira ya Maendeleo  hayo na kuifikisha kwa jamii husika.