KINONDONI
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya NAMIS CORPORATE L.T.D ambaye anajenga Soko hilo kuongeza kasi ya ujenzi huo, ili Wafanyabiashara waweze kurudi kwenye eneo lao.
Chongolo amesema hayo alipofanya ziara katika soko la Tandale na kuwakuta wafanyabiashara katika mazingira yasiyo rafiki hali inayopelekea usumbufu wa shughuli zao na kumuelekeza mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi huo, ili kuondokana na adha inayowakabili.
Amesema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha miundo mbinu yote ya masoko, ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara na kuendesha maisha yao na hivyo kuziwezesha Halmashauri kufikia malengo hayo.
Amefafanua kuwa mradi huo wa Soko la kisasa unajengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 8.7 fedha ambazo zimetolewa na Serikali kuu na kwamba tayari mkandarasi huyo ameshalipwa fedha zote na hivyo kusisitiza kwamba anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ilikukamilisha kazi yake kwa wakati.
“Serikali ya Rais Dk. John Magufuli imemlipa mkandarasi pesa zote, hivyo hatudai badala yake sisi ndio tunamdai Soko letu atukabidhi kwa wakati sahihi, wafanyabishara na wananchi wanasubria kwa shauku kubwa sana ukizingatia Soko hili nimuhimu kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwasababu litahusika zaidi na biashara ya mazao ya nafaka pamoja na bidhaa nyingine” amesema Chongolo.