NA KHAMISUU ABDALLAH

MWENDO wa kasi wa spidi 55 ya gari iliyokuwa ikiendeshwa Said Gharib Mohammed (24) mkaazi wa Kiembesamaki wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, umemsababishia kufikishwa mahakamani.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, mbele ya Hakimu Nazrat Suleiman na kusomewa mashitaka yanayomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali.

Alidaiwa kuwa, Mei 30 mwaka huu majira ya saa 5:20 za asubuhi huko Maungani, mshitakiwa huyo akiwa dereva wa gari yenye nambari za usajili Z 584 KQ P/V akitokea Kisauni kuelekea Kombeni.

Alipatikana akiwa anaendesha gari hiyo kwa mwendo wa spidi 55 km/h, mwendo ambao hauruhusiwi na kutakiwa kuendesha gari hiyo kwa spidi 40 km/h katika maeneo hayo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Sambamba na shitaka hilo, mshitakiwa huyo pia alisomewa shitaka la kusindwa kusimama baada ya kusimamishwa na askari Polisi wa kitengo cha usalama barabarani, kinyume na kifungu cha 141 (1) (a) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Koplo Salum alidai kuwa, mshitakiwa huyo siku hiyo hiyo katika maeneo hayo, alisimamishwa na askari Polisi aliekuwa kazini H 3093 PC Khatib, akiwa amevaa sare za Polisi, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Aliposomewa mashitaka hayo aliyakubali na kuiomba mahakama imsamehe, kwa kudai kuwa ndio makosa yake ya mwanzo.

Mwendesha Mashitaka Koplo Salum alidai kuwa, pamoja na kutokuwa na kumbukumbu za mshitakiwa huyo mahakamani hapo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa mashitaka aliyopatikana nayo.

Hakimu Nazrat, alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 50,000 kwa kosa la kwanza, akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki mbili, huku kosa la pili kulipa faini ya shilingi 10,000 na akishindwa atatumikia jela kwa muda huo huo.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki nne.