CCM yatangaza fungua mitambo ya ushindi 

NA SAIDA ISSA, DODOMA

MGOMBEA wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, Dk. John Magufuli amechukua fomu ya kuomba uteuzi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza katika viwanja vya makao makuu ya CCM jijini Dodoma, Dk. Magufuli alisema, ameamua kuchukua fomu yeye na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan ili wakamilishe miradi mingi ya maendeleo waliyoianza.

“Tumefanya mambo mengi katika kipindi hiki, tumejenga skuli za msingi zaidi ya 908, skuli za sekondari zaidi ya 228, vituo vya afya zaidi ya 500, mambo mengi mengi yamefanyika”, alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa; “Ukiangalia Dodoma tu, tumefanya upanuzi wa uwanja wa ndege, tumweka taa za barabarani, majengo mengi yamejengwa, kuna programu ya kujenga barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 110 ambayo imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 700”, alisema.

“Kwa hiyo nikiangalia sioni mwingine wa kuja kuyafanya hayo, tunajenga reli ya mwendokasi ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 87 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kpande cha Morogoro-Dodoma ujenzi wake umefikia asilimia 32 na tunahitaji tuendelee mpaka Mwanza”.

Vile vile alisema katika kipindi chake cha miaka mitano umeme umesambazwa katika vijiji 9,402 kutoka vijiji 3,000 wakati tunaingia madarakani, vimebaki vijiji 3,000 ambavyo alisema havitamshinda kuvifikia kwa miaka mitano.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mama Samia alimpongeza Rais Magufuli kwa kuhakikisha vifo vya akina mama na watoto vinapungua kutokana na ujenzi wa vituo vya afya nchini na pia kumpongeza kwa kasi ya usambazaji maji kwa asilimia 74.

Naye Katibu Mkuu wa CCM Dkt.Bashiru alisema, chama hicho kimewasha mitambo yake rasmi ya kutafuta ushindi kwenye uchaguzi mkuu huku akigawa majukumu kwa jumuiya za chama hicho.

“Mitambo ya kuhakikisha CCM inashinda imewashwa rasmi leo (jana), muda wa kutesti mitambo umekwisha, sasa ni kazi ya kulinda kura, kuhamasisha wapiga kura nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda kwenda kupiga kura na jukumu hili nalikabidhi kwa UVCCM,

Alizungumzia wanaodai watafanya kazi na bata huku alisema, CCM hakifanyi kazi na bata huku akisema wale wanaosema utapigiwa kura na vitu, wanajidanganya na kwamba miradi aliyoifanya ndio itakayowafanya wananchi wampigie kura kwani fedha zao ndio zimetumka kufanya miradi hiyo.

“Naomba niseme moto tutakaouwasha tusilaumiane kwa watakaobabuka, heri kwa Cheyo na Mrema walioamua kutuunga mkono, waliobaki tutambana nao”, alisema Dk. Bashiru.

Akitoa taarifa   kabla ya kukabidhi mkoba wa fomu za kugombea urais Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage alisema, mkoba huo una seti nne za fomu za uteuzi na nakala nane za fomu ya kuheshimu maadili ya uchaguzi.